Augsburg kujaribu kuipunguza kasi ya Bayern
12 Desemba 2014Mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Müller anakiri kuwa kila mara Augsburg inajikakamua sana mbele ya Bayern. Mbele ya Augsburg kila mara inakuwa hali ngumu. Wanapambana na wanajua wanachofanya, kila mahali ulinzi ama ushambuliaji. Kwa muda mrefu wamekuwa na kocha mmoja na wanatambua , kile kinachotarajiwa. Wanacheza vizuri. Kwa hiyo utakuwa mchezo mgumu. Lakini tunataka kama kawaida kushinda.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana , Augsburg iliipiga mwereka Bayern kwa bao 1-0 na hiyo ilikuwa Aprili mwaka huu, na kufikisha mwisho wa msururu wa ushindi wa Bayern wa michezo 53 katika ligi. Bayern ina pointi 12 zaidi ya Augsburg na inaongoza pia kwa pointi 7 dhidi ya timu inayoifuata VFL Wolfsburg ambayo iko nyumbani ikiikaribisha Paderborn siku ya Jumapili. Bayer Leverkusen na Borussia Moenchengladbach , zote zikiwa nyuma ya Augsburg kwa pointi moja , zinakwaana pia kesho Jumapili.
Schalke itakuwa nyumbani ikiikaribisha FC Koln leo jioni, wakati VFB Stuttgart inasafiri kwenda Mainz , na Werder Bremen ambayo ni ya pili kutoka mkiani mwa ligi inaikaribisha nyumbani Hannover na Freiburg inatiana kifuani na Hamburg SV.
Borussia Dortmund wakati huo huo inasafiri kuelekea mji mkuu Berlin ambako inasubiriwa na Hertha Berlin ambayo nayo inasua sua msimu huu pia , ikitaraji ushindi dhidi ya Hoffenheim wiki iliyopita utaanzisha msururu wa ushindi tena kama zamani. Huyu hapa kocha wa Borussia Dortmund Jürgen Klopp.
Katika michezo minne iliyopita ya Bundesliga tumeweza tu kupata pointi 7. Hali hii tunataka kuiimarisha. Mchezo wa mwisho wa hali ya kutoridhika tunataka kuutupa kwa Hertha BSC. Ambapo timu ya kocha Jos Luhukay inatambua hilo, inafahamu kwamba hali ya mapambano ya mtu na mtu inaweza kuamua mchezo huo. Tunapaswa kuwa tayari na hali hiyo, haya ni mapambano ya kujinasua kushuka daraja na sio vingine. Mtu anapaswa kutambua hilo na sisi tunatambua hilo na tunataka kuendeleza hali ya ushindi.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe , dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman