Aung San Suu Kyi aonekana hadharani kwa mara ya kwanza
24 Mei 2021Kiongozi wa timu ya mawakili wa kiongozi huyo, Khin Maung Zaw, alisema waliweza kukutana na Aung San Suu Kyi kabla ya kesi kuanza kusikilizwa na wakajadiliana naye masuala ya kisheria.
Khin aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake katika mji mkuu wa Myanmar, Naypyitaw, siku ya Jumatatu (Mei 24) kwamba mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 77 na ambaye yuko kwenye kifungo cha nyumbani tangu mapinduzi yafanyike, alikuwa na hali nzuri ya kiafya, ingawa ilibidi kwanza aulize mahala walipo, kwani hakuwa akipajuwa.
"Kwanza Kiongozi Aung San Suu Kyi aliuliza alikuwa mahala gani, nasi tukamuambia kuwa tupo kwenye uwanja wa baraza la mji wa Naypyitaw, lakini hatukujuwa nambari ya chumba. Kisha akatuambia kuwa hakuwa akijuwa alipokuwa akifungiwa," alisema Khin.
Salamu kwa wananchi
Mwanasheria mwengine anayemuwakilisha mshindi huyo wa zamani wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Min Min Soe, alisema kesi yake ilikuwa imepangiwa kusikilizwa tena tarehe 7 Juni katika mahakama maalum iliyoanzishwa kwenye mji mkuu, karibu na nyumbani kwake.
Khin alisema alikuwa amepewa salamu maalum na Aung San Suu Kyi kwa wananchi wa Myanmar, akiwatakia afya njema na kuendelea kukiunga mkono chama chake cha NLD, alichosema msingi wake ni umma.
"Kiongozi Aung San Suu Kyi amewaambia mawakili kwamba anawajali wananchi wote. Kitu kimoja alichosema ni kwamba chama chake kinakuwa kwa sababu ya watu na popote walipo watu, lazima pawe na chama," alisema Khin.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mawakili kukutana naye uso kwa macho tangu jeshi limtiye nguvuni tarehe 1 Februari, licha ya kuhudhuria vikao vya kesi yake kwa njia ya mtandao.
Mawakili pia waliweza kukutana na aliyekuwa rais wa Myanmar kabla ya mapinduzi ya kijeshi, Win Myint, ambaye anatuhumiwa pamoja na Aung San Suu Kyi kwenye baadhi ya mashitaka.
Mashitaka waliyopandishiwa kizimbani siku ya Jumatatu yalihusu kuvunja sheria ya kuzuwia kusambaa kwa maambukizo ya virusi vya corona na kuingiza simu za upepo zilizotumiwa na walinzi wake wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020 bila kibali cha serikali.