Aung San Suu Kyi huenda akashtakiwa na utawala wa kijeshi
3 Februari 2021Ripoti zilizochapishwa katika mitandao mbalimbali ya mitandao ya kijamii zinasema uongozi mpya wa kijeshi uliochukua madaraka kwa nguvu na kumkamata kiongozi wa kiraia, Aung San Suu Kyi, na viongozi wenzake wengine, unapanga kumshtaki mwanasiasa huyo kwa kosa la uhaini.
Suu Kyi alikamatwa katika mji wa Naypyidaw pamoja na Rais Win Myint na maafisa wengine wa serikali katika msako uliofanyika Jumatatu alfajiri.
Jeshi likatangza hali ya hatari na kumkabidhi madaraka mkuu wa majeshi, Min Aung Hlaing, na kisha kutangaza baraza jipya la mawaziri linalojumuisha majenerali, viongozi wa zamani wa kijeshi na wanasiasa kutoka chama kinachoungwa mkono na jeshi.
Ripoti zinaeleza kwamba Suu Kyi, wanasiasa wa chama chake cha NLD na wabunge watafunguliwa mashtaka.
Nchini Myanmar kesi ya uhaini adhabu yake inabeba kifungo cha hadi miaka 20 jela na wakati mwingine adhabu ya kifo hutolewa kwa mujibu wa gazeti moja linaloegemea upande wa serikali katika ripoti yake ya mwaka 2018.
Lawama za kimataifa zaendelea kutolewa
Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa kwa ujumla zimelitaka jeshi kuheshimu matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwaka jana Novemba, huku Marekani na Umoja wa Ulaya zikitishia kuiwekea vikwazo Myanmar, ingawa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa bado halijakubaliana kuhusu msimamo wa pamoja.
Nchini Myanmar kwenyewe, miito ya maandamano ya kiraia imeendelea kutolewa hii leo, wakati ambapo Marekani imesikika kwa mara ya kwanza ikitamka rasmi kwamba kilichofanywa na jeshi ni mapinduzi na kusema itachukua hatua zaidi dhidi ya majenerali waliohusika.
Jeshi la Myanmar linadai udanganyifu mkubwa ulifanyika katika uchaguzi uliompa ushindi San Suu Kyi na chama chake cha NLD na hiyo ndiyo sababu ya kukamatwa kiongozi huyo wa kiraia na wenzake na uongozi wa nchi kushikiliwa na jeshi.
Hatua hiyo ya mapinduzi ya kijeshi imeufikisha mwisho utawala wa kidemokrasia wa muda mfupi nchini humo.
Hasira ya umma yaanza kuonekana Myanmar
Ripoti kutoka ndani ya Myanmar zinasema kinachoonekana katika mitaa ya miji mikubwa ya nchi ni wanajeshi na magari ya kijeshi, huku idadi ndogo ya raia wakionekana katika maandamano.
Lakini dalili za wananchi kuwa na hasira zimeanza kujitokeza na mipango ya kuandamana kulipinga jeshi inapamba moto.
Madaktari na wafanyakazi wa hospitali kote nchini humo wametangaza kwamba leo Jumatano watavaa utepe mwekundu na kugoma kufanya kazi katika maeneo ambayo sio ya huduma za dharura kupinga mapinduzi.
Wanaharakati nao wametangaza kampeni ya maandamano kupitia ukurasa wa Facebook ambapo kufikia leo waliofuatilia kampeni hiyo ni watu 150,000.
Pia imeripotiwa kwamba kelele, vifijo, na ngoma, sauti za honi za magari zilirindima mji mzima wa Yangon jana jioni baada ya kutolewa kwenye mitandao ya kijamii miito hiyo ya mandamano.