1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Austin: Ukraine inaweza kuishinda Urusi

26 Aprili 2022

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ameanzisha mkutano wa masuala ya usalama na zaidi ya nchi 40 Jumanne nchini Ujerumani kwa kuelezea matumaini kwamba Ukraine inaweza kuishinda Urusi.

Deutschland | Konferenz zum Ukraine-Krieg in Ramstein
Picha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Nchi 40 zinafanya mkutano katika kambi ya kijeshi ya Marekani ya Ramstein kusini magharibi mwa Ujerumani, mkutano huo ukijikita katika kuimarisha uwezo wa kujilinda wa Ukraine. Kulingana na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, mkutano huo ambao umeitishwa na nchi yake unalenga "kufanya mambo ya ziada yatakayouongeza uwezo wa jeshi la Ukraine."

"Ukraine inahitaji msaada wetu iweze kushinda leo na bado itahitaji msaada wetu vita vitakapokwisha. Kama anavyosema Rais Biden, usaidizi wetu wa ulinzi umekwenda moja kwa moja katika mstari wa mbele wa uhuru na wapiganaji wa Ukraine wenye ujuzi na wasio na uoga. Rafiki zangu wa Ukraine, tunajua mzigo munaoubeba nyote na tunajua na nyie pia munastahili kujua kwamba sote tunawaunga mkono. Na ndio maana tuko hapa leo, kuiongezea nguvu demokrasia ya Ukraine," alisema Austin.

Ujerumani kutuma zana za kivita Ukraine

Kufuatia shinikizo na ukosoaji kutoka nyumbani na nje ya nchi kuelekea mkutano huo, serikali ya Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani sasa imeidhinisha kuisaidia Ukraine kwa zana za kivita. Haya yamesemwa na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Christine Lambrecht, katika kile kinachoonekana kama mabadiliko ya wazi ya sera ya tahadhari ya Ujerumani katika vita vya Urusi na Ukraine.

Gari la kivita aina ya Caesar CannonPicha: Vaclav Salek/CTK/dpa/picture alliance

Kulingana na hotuba iliyoonekana na shirika la habari la Ufaransa, AFP, Lambrecht ameuambia mkutano huo wa Ramstein kwamba serikali imeidhinisha kuwasilishwa kwa mizinga ya kuzia mashambulizi ya ndege nchini Ukraine.

Ufaransa kwa upande wake inawasilisha magari yaliyo na uwezo wa kurusha mizinga umbali wa kilomita 40 kwa jina Caesar Cannons nayo Uingereza inawasilisha mfumo wa ulinzi wa hewani wenye uwezo wa kuzuia makombora pamoja na mizinga.

Watu wanaendelea kuuwawa Ukraine

Wizara ya ulinzi ya Marekani imeweka wazi kwamba mkutano huo wa Ramstein haujadhaminiwa na muungano wa kujihami wa NATO kwani hata nchi ambazo si wanachama wa NATO zimealikwa.

Mkutano wa Ramstein ulioitishwa na Marekani ukiendeleaPicha: Michael Probst/AP Photo/picture alliance

Hali nchini Ukraine imesalia kuwa ya kutamausha wakati ambapo wawakilishi wa nchikadhaa walipokuwa wakielekea kuhudhuria mkutano huo huku kukukiwa na ripoti za watu kuuwawa na kujeruhiwa kote nchini humo kutokana na mashambulizi yanayoendelea ya Urusi.

Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na mwenzake wa mambo ya nje Antony Blinken walifanya ziara nchini Ukraine hapoJumapili ambapo walikutana na Rais Volodymyr Zelenskiy na kumuahidi kwamba watatoa msaada zaidi wa kijeshi kwa nchi hiyo.

Chanzo/Reuters/DPAE/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW