1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Australia na Japan zaimarisha ushirikiano wao wa kijeshi

6 Januari 2022

Viongozi wa Japan na Australia Fumio Kishida na Scott Morrison wametia saini makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi. Wakati wa hafla ya kutia saini makubaliano hayo, Kishida aliutaja mkataba huo kuwa wa kihistoria

Japan Premierminister Fumio Kishida
Picha: The Yomiuri Shimbun/AP Images/picture alliance

Makubaliano hayo yanajumuisha kupelekwa haraka kwa wanajeshi, kupunguza vikwazo dhidi ya usafirishaji wa silaha na vifaa vya mazoezi na operesheni za kukabiliana na majanga iwapo kutatokea majanga asili. Mkataba huo wa ulinzi na usalama kati ya mataifa hayo mawili unalingana na makubaliano ambayo awali Japan ilikuwa nayo na taifa la pekee lililokuwa likiilinda, Marekani.

Ushirikiano huo wa karibu wa kijeshi na Australia pia unafanyika kwa kuzingatia uwepo mkubwa wa jeshi la China katika eneo hilo. China imekosoa mkataba huo wa ulinzi.

Katika taarifa, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Wang Wenbin amesema kuwa siku zote wanaamini kuwa ubadilishanaji kati ya serikali pamoja na ushirikiano vinapaswa kusaidia katika kukuza maelewano na uaminifu miongoni mwa mataifa katika kanda hiyo na kulinda amani na utulivu wa kikanda badala ya kulenga ama kudhoofisha maslahi ya taifa lingine.

Scott Morrison - Waziri mkuu wa AustraliaPicha: UN Web TV via AP/picture alliance

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa bahari ya Pasifiki ni pana kwa maendeleo ya pamoja ya mataifa katika kanda hiyo na kwamba bado kwa kuzingatia hilo, amani na uthabiti katika eneo hilo la pasifiki inategemea juhudi za pamoja za mataifa katika eneo hilo. Wenbin ameendelea kusema kuwa anatumaini kuwa bahari hiyo ya Pasifiki itakuwa eneo la amani na wala sio la vurugu.

Mataifa ya kundi la Quad

Japan na Australia ni sehemu ya kundi la mataifa manne ya India-Pasifiki linalojulikana kama Quad ambalo pia linazijumuisha Marekani na India. Eneo la India- Pasifiki linamaanisha eneo linalotokea India hadi katika bahari ya pasifiki. Mataifa hayo manne yanataka kupanua ushirikiano wao katika eneo hilo ili kukabiliana na China.

Hivi karibuni, Kishida alisisitiza azma yake ya kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine yanayozingatia demokrasia. Tangu mwezi Oktoba, Japan imekuwa ikijadili kuhusu makubaliano sawa na hayo na Uingereza kama vile na Australia. Kwa kuongezea, taifa hilo tayari linashirikiana kwa karibu zaidi na Ufaransa katika sekta ya usalama na pia linataka kuimarisha ushirikiano na Ujerumani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW