1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Australia yaacha kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel

18 Oktoba 2022

Wapalestina wamepongeza uamuzi uliochukuliwa na Australia leo wa kubatilisha hatua ya kuutambua mji wa Jerusalem Magharibi kama mji mkuu wa Israel, licha ya kukosolewa sana na Israel.

Israel I West Jerusalem
Picha: Chris McGrath/Getty Images

Waziri wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong amesema nchi hiyo imebatilisha uamuzi wake wa awali wa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel, hatua iliyokosolewa na Israel.

Serikali ya chama cha mrengo wa kushoto cha Australia cha Labour, badala yake kimeutambua Tel Aviv kama mji mkuu wa Israel.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Australia Penny Wong amesema kuwa baraza la mawaziri la nchi hiyo pia limesisitiza kuwa hadhi ya mji wa Jerusalem inafaa kutatutiliwa kwa njia ya mazungumzo kati ya Israel na Wapalestina.

Wong amesisitiza kuwa Australia imejitolea kwa suluhisho la pande mbili katika mzozo kati ya Israel na Palestina na kuongeza kuwa nchi hiyo haitounga mkono mbinu yoyote nyengine inayokwenda kinyume na matarajio yao.

Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid ameonyesha kusikitishwa kwake na msimamo huo mpya wa Australia. Katika taarifa, Lapid amesema "Jerusalem ni mji mkuu wa milele wa Israel na kamwe hakuna lolote linaloweza kubadilisha hilo.”

Wong amesema wizara yake ilifanya makosa kwa kuweka maelezo mapya kwenye tovuti yake juu ya sera ya Australia kuhusu mji mkuu wa Israel hata kabla la baraza la mawaziri kuthibitisha mabadiliko yake ya kubatilisha uamuzi wake wa awali wa kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Hali hiyo ilisababisha mkanganyiko katika vyombo vya habari juu ya msimamo halisi wa Australia kuhusu hadhi ya mji mkuu wa Israel kabla ya tangazo la Wong.

Lapid alionekana kulaumu mkanganyiko huo wa vyombo vya habari kama chanzo cha Australia kubadilisha sera yake.

Australia imefuta maamuzi yaliyofikiwa mwaka 2018 na aliyekuwa waziri mkuu 

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Australia Scott MorrisonPicha: WILLIAM WEST/AFP

Wizara ya mambo ya nje ya Israel imesema itamuita balozi wa Australia kuelezea masikitiko yake juu ya uamuzi huo ambao umeutaja kama uliochukuliwa kwa kuzingatia kile ilichokiita fikra fupi za kisiasa.

Waziri wa masuala ya ndani ya mamlaka ya Wapelastina Hussein al Sheikh amesema kupitia ujumbe wa Twitter, wanaukaribisha uamuzi wa Australia kuhusu Jerusalem na mwito uliotolewa na nchi hiyo wa kutaka suluhisho la kuundwa madola mawili kwa mujibu wa sheria ya kimataifa.

Hatua ya sasa ya Australia imefuta maamuzi yaliyofikiwa mwaka 2018 na aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Scott Morrison aliyeunga mkono uamuzi uliochukuliwa na rais wa Marekani wakati huo Donald Trump japo ofisi za ubalozi wa Australia bado zimesalia mjini Tel Aviv.

 

  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW