1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Australia yawaomba radhi watoto walionyanyaswa kingono

22 Oktoba 2018

Waziri Mkuu wa Australia, Scott Morrison amewaomba radhi waathirika walionyanyaswa kingono wakati wakiwa watoto, akisema kuwa taifa hilo lilishindwa kuwalinda.

Australien Parlament Scott Morrison Entschuldigung Missbrauchsopfer
Picha: Getty Images/AFP/S. Davey

Akizungumza kwa hisia wakati akilihutubia bunge hii leo, Morrison amesema taifa lake lilishindwa kuwalinda watoto hao dhidi ya uhalifu wa kingono uliokuwa wa kutisha ambao ulifanywa miongo kadhaa iliyopita na kwamba hiyo ni aibu kubwa kwa Australia. Amesema wanakiri makosa yao kwa kushindwa kuwasikiliza, kuwaamini na kutoa haki kwa watoto.

''Leo serikali ya Australia na bunge hili kwa niaba ya watu wote wa Australia, nawaomba msamaha waathirika na walionusurika na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto. Kwa miaka mingi macho na mioyo yetu iliufumbia macho ukweli tulioambiwa na watoto,'' alisema Morrison.

Ombi hilo la msamaha liliooneshwa moja kwa moja kupitia televisheni, ni mojawapo ya mwongozo wa uchunguzi wa miaka mitano, uliobaini kuwepo kwa kiwango kikubwa cha kutisha cha uhalifu wa kingono uliofanywa dhidi ya watoto katika taasisi za kidini na serikali zaidi ya miaka 90 iliyopita.

Katika visa vingi, uhalifu huo ulifanywa na mapadri, waangalizi wa vituo vya kuwalea watoto yatima pamoja na watu wengine waliokuwa na mamlaka.

Watu wakimfatilia kwenye televisheni Waziri Mkuu Scott Morrison akiomba msamahaPicha: Getty Images/AFP/S. Davey

Tume iliyofuatilia na kuchunguza visa vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, ilisema kuwa ilizishughulikia zaidi ya kesi 15,000 za unyanyasaji wa kingono na kusikiliza ushahidi kutoka kwa kiasi ya watu 8,000 walioathirika. Tume hiyo ndiyo iliyofanya kazi kwa muda mrefu zaidi nchini Australia.

Morrison amesema atafungua makumbusho ya taifa kuhamasisha kuhusu madhara makubwa yatokanayo na unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto.

Amesema watafanya kazi kwa pamoja na makundi ya waathirika ili kuhakikisha visa vyao vinaandikwa, ukweli unaelezewa wazi, ili taifa la Australia lisiikimbie aibu yake na kwamba hawatosahau uhalifu huo uliotendeka dhidi yao.

Mamia ya waathirika pamoja na familia zao walikusanyika mjini Canberra na katika mapokezi maalum ya nchi nzima, kushuhudia tukio hilo la kuomba msamaha.

Richard Jabara, mmoja wa waathirika ambaye alinyanyaswa na padri katika miaka ya 1970 alikuwa akilia muda wote wakati Waziri Mkuu Morrison akiomba radhi.

Taasisi kadhaa za Australia likiwemo Kanisa Katoliki cha chama cha Maskauti zimeomba radhi kwa kushindwa kuwalinda watoto katika vituo vyao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ DPA, AP, AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga