1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Austria yaanza zuio jengine kupambana na COVID-19

22 Novemba 2021

Austria imeanza rasmi zuio la shughuli za kawaida za maisha ili kukabiliana na wimbi la nne la maambukizo ya virusi vya corona, siku moja baada ya miji kadhaa barani Ulaya kushuhudia maandamano makubwa ya umma.

Österreich Corona-Maßnahmen Protest-
Picha: Vadim Ghirda/dpa/AP/picture alliance

Austria ilianza rasmi mapema ya siku ya Jumatatu (Novemba 22) kutekeleza amri ya kuzuwia baadhi ya shughuli muhimu za maisha, baada ya wiki kadhaa za kushuhudia idadi ya wanaopoteza maisha kila siku kutokana na COVID-19 ikipanda.

Baadhi ya hospitali zikionya kwamba uwezo wa vyumba vyao vya wagonjwa mahututi unakaribia kufikia ukomo wake.

Zuio la sasa lilipangwa kuendelea kwa siku 10 lakini upo uwezekano wa kuongezwa hadi 20, ambapo watu wanaruhusiwa tu kutoka majumbani mwao wakiwa na sababu za msingi, kama vile kununuwa vyakula, kumuona daktari ama kufanya mazoezi. 

Amri hii ilikwenda sambamba na tangazo la Ijumaa (Novemba 19) la Waziri Mkuu Alexander Schallenberg kwamba chanjo dhidi ya virusi vya corona itakuwa jambo la lazima kufikai tarehe 1 Februari. 

Maandamano kote Ulaya

Maandamano mjini Amsterdam.Picha: Eva Plevier/REUTERS

Kwengineko barani Ulaya, miji kadhaa ilishuhudia maandamano ya maelfu ya watu siku ya Jumapili (21 Novemba) wanaopinga uwezekano wa mataifa yao kutangaza marufuku nyengine ya shughuli za kimaisha katika vita dhidi ya virusi hivyo. 

Katika mji wenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya, Brussels, waandamanaji walipaza sauti zao kupinga hatua mpya za vizuizi vilivyowekwa na serikali ya Ubelgiji. 

Waandamanaji hao walidai kwamba wanataka uhuru wao wa kuyaishi maisha bila kubaguliwa kwa sababu ya chanjo ya corona, kwani uhuru ndio msingi ya maadili ya Kimagharibi.

"Kimsingi tunataka uhuru wetu. Kuchomwa chanjo kwa kitu kisichofanyiwa majaribio vyema, kutoweza kufanya kazi unapotaka, kuwa utakapo, hayo siyo maadili yetu, huo sio uhuru, hivyo sivyo tunavyoishi. Tunaishi Ulaya ya Magharibi na tunataka uhuru wetu tu, kama tulivyokuwa nao kabla," alisema Eveline Denayer, mmoja wa waandamanaji hao mjini Brussels.

Maandamano dhidi ya ubaguzi

Maandamano mjini Brussels.Picha: Olivier Matthys/AP Photo/picture alliance

Waandamanaji wengine walisema wanapinga kile walichosema ni ubaguzi na ukosefu wa usawa barani Ulaya, ambapo watu waliochanjwa na wasiochanjwa wanatenganishwa kwa makusudi.

"Nipo hapa... sijui namna ya kuelezea, nipo hapa kupinga ubaguzi. Watu wanabaguliwa kwa sababu ya msimbo. Watu washaochanjwa hawawezi kuingia majengo mengine kwa kuwa wamechanjwa mara moja... Hii ndiyo sababu tupo hapa, watu wanabaguliwa, hatulitaki jambo hili," alisema mwandamanaji mwengine, Kenny Du Coq.

Polisi inakisia kuwa watu 35,000 tayari walishaondoka kwenye maandamano hayo kurejea majumbani, pale vurugu zilipozuka kwa watu kuvunja magari, kuwashambulia polisi na kumwaga madebe ya taka.

Kwa uchache, kuna ripoti ya maafisa watatu wa polisi na muandamanaji mmoja kujeruhiwa kwenye makabiliano hayo.

Maandamano yalifanyika pia katika miji kadhaa ya Uholanzi, Denmark na hapa Ujerumani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW