Uchaguzi wa Papa waingia siku ya pili Vatican
8 Mei 2025
Waumini hao wamekusanyika baada ya Makadinali kurejea katika Kanisa la Sistine Alhamisi 08.05.2025 katika duru ya pili ya kura itakayoamua juu ya Kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki.
Awamu ya pili ya uchaguzi wa Papa inafanyika saa kadhaa baada ya moshi mweusi ulioonekana Jumatano ishara kuwa mrithi wa kiongozi huyo bado hajapatikana.
Soma zaidi: Makadinali washindwa kumchagua papa mpya katika duru ya kwanza
Makadinali wanafanya mchakato huo wa siri wa kumchagua kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki atakayewaongoza waumini bilioni 1.4. Kongamano la viongozi hao wa Kikatoliki waliojitenga ili kuepusha uchaguzi wa Papa kuingiliwa, ndiyo kubwa zaidi na lenye sura ya kimataifa, linalowaleta pamoja makardinali 133 kutoka karibu nchi 70.
Linafanyika wakati mji wa Vatican na maeneo yanayouzunguka yakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi, na maafisa wengine wa usalama. Kulingana na uongozi wa Vatican ngwe mpya ya kura ilitarajiwa kuanza majira ya saa tatu asubuhi. Kuonekana kwa moshi mweupe baada ya kura ya awamu ya pili kutaashiria kuwa kiongozi mya wa kanisa hilo amepatikana.
Matumaini ya kumpata mrithi wa Papa Francis siku ya pili ya uchaguzi
Hata hivyo katika zama hizi, hakuna Papa ambaye amewahi kuchaguliwa katika awamu ya kwanza. Kwa kuzingatia historia ya miaka ya hivi karibuni matokeo ya mwisho yanaweza kuamuliwa katika siku ya pili ya kura ambayo ina nafasi ya kuwa na awamu nne za kupiga kura.
Wakiwa wamevalia kofia nyekundu, viongozi hao wa kanisa walitazamiwa kupiga kura katika awamu mbili asubuhi, na awamu nyingine ya kura imepangwa kupigwa mchana na wataendelea siku hzijazo hadi pale mtu mmoja atakapopata theluthi mbili ya kura zote, itakayompa ridhaa ya kuwa Kiongizi wa 267 wa Kanisa Katoliki duniani.
Katika uchaguzi huo, Kadinali Pietro Parolin raia wa Italia aliyefanya kazi kama kiongozi nambari mbili baada ya Papa Francis, pamoja na Kardinali wa Ufilipino Luis Antonio Tagle wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kushinda kwenye mchakato huo.