1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ayatullah Ali Khamenei atetea kuishambulia Israel

4 Oktoba 2024

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, leo ametoa hotuba ya nadra wakati wa ibada ya siku ya Ijumaa ambayo ameitumia kutetea shambulizi la makombora la nchi yake dhidi ya Israel la mnamo Oktoba Mosi.

Iran | Khamenei
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, akihutubia maelfu ya waumini wa Kiislamu kwenye sala ya Ijumaa siku ya tarehe 4 Oktoba 2024 mjini Tehran.Picha: IRNA Agency

Kwenye hotuba hiyo mbele ya mamia kwa maelfu ya watu waliokusanyika kwenye msikiti mkuu wa Imam Khomeini Mosalla mjini Terhan, Khamenei amesema shambulizi lililoilenga Israel lilikuwa halali kisheria na kwamba upinzani dhidi ya dola hiyo hautakoma. 

Kiongozi huyo mkuu Iran pia ameyasifu makundi ya Hezbollah na Hamas yanayopigana na Israel nchini Lebabon na Ukanda wa Gaza, akisema yanafanya hivyo kulinda maslahi ya kanda nzima.

Soma zaidi: Iran yawaita mabalozi wa Ulaya baada ya kuikosoa kufuatia shambulizi lake dhidi ya Israel

Makundi hayo mawili yameorodheshwa kuwa ya kigaidi kwenye mataifa mengi ya Magharibi na Israel inaendesha kampeni ya kijeshi inayodai ina nia ya kuyasambaratisha. 

Hotuba ya Khamenei wakati wa ibada ya Ijumaa ambayo ni ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano, imetolewa wakati wasiwasi unaongezeka kwamba kanda ya Mashariki ya Kati ipo ukingoni wa kutumbikia kwenye vita kamili.