1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Wanajeshi 192 wa Azerbaijan wameuawa Nagorno-Karabakh

27 Septemba 2023

Serikali ya Azerbaijan imesema kuwa jumla ya wanajeshi 192 wameuawa na wengine 511 wamejeruhiwa wakati wa operesheni ya kijeshi ya wiki iliyopita kwenye eneo la Nagorno-Karabakh.

Aserbeidaschan | Berg-Karabach | nach Militäraktion beschlagnahmte Waffen und Ausrüstungsgegenstände
Picha: REUTERS

Wizara ya Afya ya Azerbaijan imetangaza Jumtano kuwa raia mmoja pia ameuawa katika mapigano hayo. Awali maafisa wa Nagorno-Karabakh walisema kuwa takribani watu 200 wa upande wao, wakiwemo raia 10 waliuawa na wengine zaidi ya 400 walijeruhiwa.

Operesheni hiyo ya kijeshi iliiruhusu Azerbaijan kuchukua tena udhibiti kamili wa eneo hilo lililojitenga, ambalo limekuwa likiendeshwa na watu wanaotaka kujitenga kwa miaka ipatayo 30.

Maelfu ya Waarmenia wameingia Armenia 

Waarmenia 28,000 ambao ni zaidi ya theluthi moja ya idadi ya watu 120,000 wa jimbo hilo, tayari wameondoka kuelekea Armenia

Armenia imesema Jumatano kuwa wakimbizi 42,500 wamevuka mpaka na kuingia nchini humo wakitokea Nagorno-Karabakh, wakikimbia kile ambacho kimetajwa kuwa hofu ya Azerbaijan kulipa kisasi kwa kuwafanyia vitendo vya kikatili.

Waarmenia kutoka Nagorno-Karabakh wakiondoka kwenye eneo hiloPicha: Vasily Krestyaninov/AP Photo/picture alliance

Siku ya Jumapili, Azerbaijan ilifungua barabara pekee inayotoka kwenye eneo hilo kuelekea Armenia, siku nne baada ya waasi kukubali kuweka chini silaha kwa masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano ambayo yanaliweka eneo hilo linalozozaniwa chini ya udhibiti wa Baku.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock ameitolea wito Azerbaijan kuruhusu waangalizi wa kimataifa kuingia kwenye eneo la Nagorno-Karabakh.

Ujerumani kushirikiana na washirika wake

Katika taarifa yake iliyotolewa Jumatano, Baerbock amesema Ujerumani na washirika wake wanashirikiana na kuongeza bidii ya kupeleka waangalizi haraka iwezakanavyo.

Kwa mujibu wa Baerbock, Ujerumani itaongeza msaada wake wa kiutu katika Kamati ya Kimataifa ya Shirika la Msalaba Mwekundu, ICRC, kutoka euro milioni 2 hadi 5. Amesema kuruhusu ujumbe wa waangalizi wa kimataifa itakuwa uthibitisho tosha na wenye iman kwamba Azerbaijan imejitolea kwa usalama na ustawi wa watu katika eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Armenia, Ararat MirzoyanPicha: Bebeto Matthews/AP Photo/picture alliance

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken pia amesisitiza umuhimu wa ujumbe wa kimataifa na msaada wa kiutu kuingia Nagorno-Karabakh. Msemaji wa wizara hiyo, Matthew Miller amesema Blinken ameitoa kauli hiyo Jumanne wakati akizungumza na Rais wa Azerbaijan, Ilham Aliyev.

''Waziri Blinken amezungumza tena na Rais Aliyev, na kusisitiza udharura wa kutokuwepo tena uhasama, kwamba kuwe na ulinzi usio na masharti na uhuru wa kutembea kwa raia, na huduma za kiutu ziweze kupatikana Nagorno-Karabakh,'' alifafanua Miller.

Rais Aliyev: Haki za Waarmenia zitaheshimiwa

Katika mazungumzo yake na Blinken, Rais Aliyev amesema kuwa haki za Waarmenia zitaheshimiwa.

Armenia and Azerbaijan zimepigana vita mara mbili kuligombania jimbo hilo katika kipindi cha miaka 30, huku Azerbaijan ikifanikiwa kujinyakulia maeneo mengi ya ndani na karibu na Nagorno-Karabakh, katika mzozo uliodumu kwa wiki sita, mnamo mwaka 2020.

(AP, AFP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW