1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAzerbaijan

Azerbaijan yasitisha mazungumzo ya amani na Armenia

25 Novemba 2022

Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan amesema nchi yake haitaki Ufaransa ishiriki katika mazungumzo ya amani na Armenia, na hivyo kufutilia mbali mkutano uliopangwa kufanyika mjini Brussels Desemba 7.

Tschechien Prag | Gründungsgipfel Europäische Politische Gemeinschaft | Michel, Pashinyan, Macron, Aliyev
Picha: Presidency of Azerbaijan/Handout/Anadolu Agency/picture alliance

Aliyev alisema siku ya Ijumaa (Novemba 25) kwamba Macron "ameishambulia" na "kuitusi" Baku na hapaswi kuwa kama mpatanishi.

Mapigano yalipamba moto mnamo mwezi Septemba kati ya nchi hizo mbili zilizokuwa zamani katika uliokuwa Umoja wa KiSovieti kufuatia mzozo wao wa miongo kadhaa juu ya eneo la Nagorno-Karabakh ambalo linatambuliwa kimataifa kama sehemu ya Azerbaijan, lakini kwa kiasi kikubwa linadhibitiwa na Waarmenia wa asili na kuungwa mkono na Yerevan.

Nyumba iliyobomolewa katika mzozo kati ya Azerbaijan na Armenia katika mji wa VardenisPicha: Alexander Patrin/TASS/dpa/picture alliance

Pande hizo mbili zilishutumiana kwa kuanzisha mapigano ya hivi punde ambapo Armenia ilisema Azerbaijan imenyakua makazi ndani ya mipaka yake. Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliafikiwa mwishoni mwa mwezi Septemba na mwezi uliopita mjini Prague, nchi hizo mbili zilikubali na kuruhusu ujumbe wa kiraia wa Umoja wa Ulaya kuwekwa kwenye mpaka wao wa pamoja.

Soma zaidi:Armenia na Azerbaijan zakubaliana kusitisha mapigano 

Lakini, akizungumza siku ya Ijumaa, Aliyev alimshutumu Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan kwa kujaribu kuvuruga hatua inayofuata ya mazungumzo na kusisitiza kuwa Ufaransa lazima iwe mpatanishi.

Rais Ilham Aliyev wa AzerbaijanPicha: The Presidential Office of Ukraine

Aliyev alisema wakati akizungumza kwa lugha ya Kiingereza kwenye mkutano pamoja na wawakilishi wa kimataifa mjini Baku kuwa Macron aliishambulia Azerbaijan na kuwatuhumu kwa kitu ambacho hawakufanya.

Soma zaidi: Putin azitaka Armenia na Azerbaijan kujizuia na mapigano

Aliyev amesema kiongozi huyo wa Ufaransa amedhihirisha msimamo wa kuipinga Azerbaijan na ilikuwa "tusi" kwa Baku. Aliyev amesema pia: "Ni wazi kuwa chini ya hali hizi, na mtazamo huu, Ufaransa haiwezi kuwa sehemu ya mchakato wa amani kati ya Azerbaijan na Armenia."

Armenia yakanusha madai ya Azerbaijan

Kwa upande wake wizara ya mambo ya nje ya Armenia ilisema inataka kudumisha

muundo wa majadiliano ya Prague ambayo yalimhusisha Macron na Michel.

Shirika la habari la Interfax liliripoti kuwa msemaji wa wizara hiyo amesema madai ya Azerbaijan kwamba Yerevan ilikuwa inajaribu kuvuruga mazungumzo ya amani, hayana ukweli wowote.

Nikol Paschinjan, Waziri Mkuu wa ArmeniaPicha: Karen Minasyan/AFP/Getty Images

Akizungumza kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan, Macron ameishutumu Urusi kwa kuchochea uhasama kati ya Baku na Yerevan, na pia amethibitisha uungaji mkono wake kwa uhuru wa Armenia.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya kutuma ujumbe wake Armenia

Armenia pia ilisema siku ya Ijumaa kwamba Azerbaijan haijatoa jibu kwa mapendekezo yake ya hivi karibuni ya makubaliano ya amani, ambayo iliyawasilisha katika mkutano wa mawaziri wao wa mambo ya nje mjini Washington mwanzoni mwa mwezi Novemba.

Msemaji wa Kremlin Dmitry PeskovPicha: ITAR-TASS/IMAGO

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Ijumaa hii kuwa Moscow, ambayo ilipeleka vikosi vya walinda amani wapatao 5,000 katika eneo hilo mnamo mwaka 2020 ili kusimamia hatua ya usitishaji mapigano baada ya vita vya wiki sita, ilikuwa tayari kusaidia kupatikana kwa makubaliano zaidi, lakini kwamba hapakuwa na mpango madhubuti wa viongozi hao kukutana huko Moscow.

Soma zaidi: Pelosi alaani mashambulizi ya Azerbaijan dhidi ya Armenia

Urusi ni mshirika rasmi wa Armenia lakini pia inataka kudumisha uhusiano mzuri na Azerbaijan, na hadi sasa haijajibu wito wa kupelekwa vikosi vya kuisaidia Yerevan chini ya makubaliano ya ulinzi wa pande zote baada ya mapigano yaliyozuka mnamo mwezi Septemba.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW