1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azerbaijan yasitisha operesheni baada ya Waarmenia kusalimu

20 Septemba 2023

Azerbaijan imetangaza kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika eneo linalozozaniwa la Nagorno-Karabakh, baada ya vikosi vya Waarmenia kukubaliana kuweka silaha zao chini na kufanya mazungumzo ya kuwajumuisha tena.

Nagorno-Karabakh | Wanajeshi wa Urusi wakiondoa raia
Wanajeshi wa Urusi wakiondoa raia kutoka Nagorno-Karabakh, kufuatia operesheni kali y akijeshi ya Azerbaijan.Picha: Russian Defence Ministry/TASS/IMAGO

Chini ya makubaliano yaliothibitishwa na pande zote mbili na yanayoanza kutekelezwa jioni ya Jumatano, vikosi vya wanaotaka kujitenga vitavunjwa na kusalimisha silaha zao, na mazungumzo juu ya mustakabali wa mkoa huo na jamii ya Waarmenia wanaoishi huko yataanza siku ya Alhamisi. 

Baku na mamlaka ya Waarmenia huko Karabakh wamesema makubaliano ya kusitisha uhasama yamesimamiwa na walinda amani wa Urusi ili kusitisha mapigano siku moja baada ya Azerbaijan kuanzisha "operesheni ya kupambana na ugaidi."

Soma pia: Nagorno-Karabakh: Azerbaijan yathibitisha usitishaji mapigano

Wanaotaka kujitenga wamesema wamejitolea "kuvunja kikamilifu" vikosi vyao na kuondoa vitengo vya jeshi la Armenia kutoka eneo hilo, katikati mwa vita viwili kati ya Armenia na Azerbaijan tangu kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti.

Karabakh, ambalo ni eneo la milima lililoko katika kanda kubwa ya Caucasus Kusini, inatambulika kimataifa kama sehemu ya Azerbaijan, lakini sehemu yake imekuwa chini ya mamlaka ya Waarmenia wanaotaka kujitenga, wanaodai eneo hilo ni la mababu zao.

Mkuu wa idara ya habari ya wizara ya mambo ya ndani ya Azerbaijan Elshad Hajiyev akizungumza katika mkutano wa habari kuhusu operesheni ya kijeshi dhidi ya ugaidi huko Nagorno-Karabakh, Septemba 20, 2023.Picha: globallookpress/picture alliance

Azerbaijan, ambayo ilituma vikosi vikisaidiwa na mashambulizi ya makombora kwenda Karabakh siku ya Jumanne, katika jaribio la kulilaazimisha kutii, imesema inapanga kuwajumuisha Waarmenia 120,000 wa eneo hilo na kwamba haki zao zitalindwa chini ya katiba.

Pashinyan asema Armenia haikushirikishwa

Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan amesema katika hotuba ya televisheni kwamba mapigano yanaonekana kupungua kwa kiasi kikubwa na kusisitiza kuwa ni "muhimu sana" kwa usitishaji huo wa mapigano kuendelea.

Soma pia: Azerbaijan yaitaka Armenia kuondosha wanajeshi Nagorno-Karabkh

Waziri Mkuu Pashinyan amerudia kukanusha kuwa jeshi la nchi yake liko katika eneo hilo na kusema anatarajia askari wa kulinda amani wa Urusi kuhakikisha wakaazi wa kabila la Karabakh-Armenia wanaweza kukaa majumbani mwao, na kwenye ardhi yao.

Kuporomoka kwa upinzani wa wanaotaka kujitenga kunawakilisha ushindi mkubwa kwa Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev katika azma yake ya kuirejesha Nagorno-Karabakh yenye Waarmenia wengi chini ya udhibiti wa Baku.

Mzozo huu wa hivi karibuni unakuja miaka mitatu baada ya Azerbaijan kurejesha maeneo mengi ndani na nje ya eneo hilo katika vita vifupi vilivyoshuhudia kushindwa vibaya kwa Armenia.

Baku ilisema Jumatano kuwa imechukuwa udhibiti wa maeneo zaidi ya 60 ya kijeshi wakati wa mashambulizi hayo inayoyaita "hatua za ndani za kupambana na ugaidi."

Miito ya kusitisha mapigano

Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan amekabiliwa na maandamano nyumbani baada ya Azerbaijan kufanya mashambulizi makali Nagorno-Karabakh.Picha: Tigran Mehrabyan/PAN/AP/picture alliance

Tangazo la kusitisha mapigano limekuja baada ya Rais Aliyev kuonya kuwa operesheni ya kijeshi itaendelea hadi wale wanaotaka kujitenga waweke chini silaha zao, katikati mwa shinikizo la kimataifa la kusitisha mapigano.

Soma pia: Armenia, Azerbaijan zaelekea kupata suluhu ya Nagorno-Karabakh

Urusi, Umoja wa Mataifa na Papa Francis waliongeza miito ya kusitisha ghasia, baada ya Marekani na Ufaransa kuwasiliana na viongozi wa Azerbaijan na Armenia.

Duru hii mpya ya mapigano inakuja wakati Moscow, ambayo ndiyo taifa lenye ushawishi mkuwa katika eneo hilo, inakabiliwa na kuelekeza nadhari kwa vita vyake dhidi ya Ukraine, ambavyo vimeiacha ikiwa imetengwa na mataifa Magharibi.

Lakini walinda amani wake walioko eneo hilo walionekana kuwa na jukumu muhimu katika kusaidia mazungumzo ya kusitisha mapigano na sasa watasimamia utekelezaji wake.

Chanzo: Mashirika
 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW