1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza Kuu la UN lalaani Urusi kunyakua maeneo ya Ukraine

Daniel Gakuba
13 Oktoba 2022

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuunga mkono azimio linalolaani hatua ya Urusi kuyanyakua maeneo ya kusini na mashariki mwa Ukraine.

Symbolbild I UN - Mehrheit verurteilt Annexionen Moskaus
Nchi nyingi wanachama wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wameunga mkono azimio la kuilaani UrusiPicha: Cia Pak/UN Photo/ Xinhua/picture alliance

Nchi 143 zimeliunga mkono azimio hilo, huku nne tu zikilipinga, na nyingine 35, zikiwemo China, India, Pakistan na Afrika Kusini zimejizuia. Nchi nne zilizojiunga na Urusi kulipinga azimio hilo ni Korea Kaskazini, Belarus, Syria na Nicaragua.

Soma zaidi: Watu wanane wauawa baada ya Urusi kushambulia soko Ukraine

Awali Urusi ilishindwa katika juhudi zake za kutaka kura hii ipigwe kwa siri. Kabla ya kura hiyo kupigwa, Marekani ilifanya juhudi kubwa za kidiplomasia kuzishawishi Afrika Kusini na India ziunge mkono azimio hilo lakini haikufanikiwa.

China ambayo ni mshirika wa kimkakati wa Urusi, imesema kura hiyo ilikuwa na sura ya vita baridi na haina tija.

Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa, Sergiy KyslytsyaPicha: Seth Wenig/AP Photo/picture alliance

Washirika wa Ukraine washangilia

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas Greenfield amesema inapeleka ujumbe kwamba dunia haitavumilia tabia ya nchi moja kuyachukua kwa nguvu maeneo ya majirani zake.

Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa Sergiy Kyslytsya amesema matokeo ya kura hii ni ya ''kupendeza'' na ya ''kihistoria'', huku balozi wa Umoja wa Ulaya Olof Skoog akisema ni ''mafanikio makubwa'' ambayo ni ''ujumbe kwa Urusi kuwa imetengwa.''

Soma zaidi:  Kwa nini Daraja la Kerch ni muhimu kwa Urusi na Ukraine?

Hii ndio kura katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ambayo imeungwa mkono na nchi nyingi zaidi, kati ya nne ambazo tayari zimefanyika katika baraza hilo tangu Ursui kuivamia Ukraine mwezi Februari.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin (katikati) akiwa na wakuu wa majimbo ya Ukraine yaliyonyakuliwa kupitia 'kura ya maoni' iliyochukuliwa na nchi za magharibi kuwa batiliPicha: Grigory Sysoyev/AP Photo/picture alliance

Urusi yatoswa na baadhi ya wapambe wake

Miongoni mwa nchi ambazo zimeliunga mkono azimio hilo bila kutarajiwa ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na mataifa mengine wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba, pamoja na Brazil.

Azimio lililoungwa mkono lilipendekezwa na nchi za magharibi baada ya Urusi kuitangaza mikoa minne ya mashariki na kusini mwa Ukraine kuwa sehemu yake kufuatia ilichokiita kura ya maoni, ambayo Ukraine na washirika wake wa magharibi walisema ni batili.

Soma zaidi: Baraza la juu la Bunge la Urusi laridhia unyakuzi wa majimbo manne ya Ukraine 

Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzia alikuwa amezihimiza nchi kulipinga azimio hilo, akisema ni ''hati ya kisiasa ambayo inaonyesha uchokozi wa wazi'', na kuongeza kuwa ni ''kitisho cha watu wa magharibi wasio na maadili.'' Balozi huyo amesema inasikitisha kuwa kura hiyo haikupigwa kwa siri kama ilivyotakiwa na Urusi.

Vyanzo: dpae, rtre

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW