1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la Lugano la kuijenga upya Ukraine latiwa saini

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
5 Julai 2022

Washiriki kwenye mkutano wa kimataifa wa kuisaidia Ukraine baada ya nchi hiyo kuharibiwa kutokana na uvamizi wa Urusi wameainisha mfululizo wa kanuni za ujenzi mpya wa nchi hiyo.

Ukraine Recovery Conference | Lugano, Schweiz
Picha: Michael Buholzer/KEYSTONE/AFP/Getty Images

Wakihitimisha mkutano wa siku mbili katika jiji la kusini mwa Uswizi la Lugano, viongozi kutoka nchi zaidi ya 40 na mashirika ya kimataifa kama vile benki ya uwekezaji ya Ulaya na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo (OECD) wametia saini azimio la Lugano linaloweka kanuni za kuijenga upya Ukraine.

Ahadi zimekaribishwa kwa furaha

Wawakilishi kwenye mkutano huo pia wamekaribisha ahadi za kutoa misaada ya kisiasa, kifedha na kiufundi na wakati huo huo wamezindua kanuni za Lugano zitakazoongoza juhudi za ujenzi, ambao Ukraine inasema unaweza kugharimu hadi dola bilioni 750.

Kanuni hizo zinajumuisha ushirikiano kati ya Ukraine na washirika wake wa kimataifa na zinazingatia mageuzi ya ndani. Nchi nyingi zimeazimia kuiunga mkono Ukraine kupitia kile kinachotarajiwa kuwa ni ahueni ya muda mrefu na ya gharama kubwa, na zimekubaliana juu ya mahitaji ya mageuzi mapana ili kuongeza uwazi na vita dhidi ya ufisadi.

Rais wa Tume ya Ulaya, Ursula Von der LeyenPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Umoja wa Ulaya umesema Ukraine bado inahitaji kufanya maendeleo katika maeneo kama utawala wa sheria, kuwadhibiti matajiri wachache kwenye utawala, kuondoa upendeleo katika kutoa zabuni kwenye miradi ya ujenzi, kupambana na rushwa na kuhakikisha haki za msingi.

Miongoni mwa nchi zilizotia saini

Miongoni mwa nchi zilizotia saini azimio hilo ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ufaransa na Japan na wakati huohuo nchi hizo zimelaani uvamizi wa kijeshi wa Urusi dhidi ya Ukraine na ziitaka Moscow iondoe wanajeshi wake kutoka kwenye ardhi ya Ukraine mara moja.

Rais wa Uswisi Iganzio Cassis, aliyeandaa mkutano huo pamoja na Ukraine, katika hafla ya kuufunga mkutano huo amepongeza azimio lililofikiwa na amesema ni hatua muhimu ya kwanza katika njia ndefu ya kuirejesha Ukraine kwenye hali yake ya kawaida.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uharibifu wa nyumba, shule, hospitali, na miundombinu mingine muhimu itachukua miaka kadhaa kujengwa upya.

Kushoto: Rais wa Tume ya Ulaya Ursula Von der Leyen. Katikati: Rais wa Uswisi Ignazio Cassis. Kulia: Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal.Picha: Michael Buholzer/AFP

Guterres ameongeza kusema kuwa wajibu wa Umoja wa Mataifa ni kuiunga mkono serikali ya Ukraine katika shughuli za  kuokoa maisha, kuimarisha juhudi za kutoa misaada, kuendeleza mpango wa uokoaji na maendeleo wa Ukraine, na kulinda mafanikio yaliyopatikana kuelekea malengo ya maendeleo endelevu.

Azimio hilo la Lugano linajikita katika kujitolea kwenye mchakato wa kidemokrasia utakaohusisha sehemu zote za kijamii. Malengo yakiwa ni pamoja na kuibadilisha Ukraine kuwa mahala pa jamii iliyo kwenye mazingira safi yasiyo na hewa ukaa, na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kidijitali.

Vyanzo: AFP/RTRE/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW