1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AZIMIO LA UMOJA WA MATAIFA JUU YA IRAQ

Ramadhan Ali9 Juni 2004

GAZETINI 09-06-04

Wahariri wa magazeti ya ujerumani leo hii wamechambua maafikiano yaliofikiwa jana katika Baraza la Usalama la UM juu ya azimio jipya kuhusu Iraq lakini pia hali ya soko la kazi nchini Ujerumani kufuatia kutangazwa kwa tarakimu za mwezi uliopita .

Kuhusu muafaka uliofikiwa katika Baraza la Usalama la UM juu ya Iraq,gazeti la kusini mwa Ujerumani-SÜDDEUTSCHE ZEITUNG kutoka Munich laandika:

"Mjini Baghdad hautapita muda itadhihirika dhahiri-shahiri kwamba azimio hilo jipya la Baraza la Usalama lina kasoro zake:Kasoro yenye ni swali muhimu linalozusha mbishano.Wakati wamarekani wanashikilia kuwa na kauli ya mwisho kuhusu matumizi ya majeshi yao huko Iraq , nchi kama Ufaransa zikipendekeza kuwa serikali ya mpito ya Irak binafsi ipatiwe alao kura ya turufu (veto) kuweza kutia munda matumizi makubwa ya majeshi yaliopo nchini mwake.

Azimio lililopitishwa jana linasema majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani pamoja na serikali ya Baghdad yatashirikiana katika kila swali linalohusiana na usalama. Hii ina maana gani pakizuka mvutano ?

Kitatokea nini iwapo majeshi ya Marekani yakitaka kuukomboa mji uliotekwa na kiongozi wa wanamgambo wa-kiirak na serikali ya mpito ya Irak inapinga jambo hilo ?Nani hapo ataamua ? Hapo itabainika kwamba mamlaka nchini Amerika kama hapo kabla ya azimio yamo mikononi mwa Marekani. Ukweli huu waweza ukachochea moto upya na jazba miongoni mwa wairaki"-

Gazeti linaloonesha matumaini kidogo ni lile la jiji la Cologne: KÖLNER STASDT-ANZEIGER:Laandika-

"Ni wazi kabisa kuwa azimio hilo pekee halitatui matatizo yote na halitailetea amani Irak.Lakini ni azimio linaloipa jamii ya kimataifa jukumu kuchangia kuisindikiza Irak kutoka kipindi hiki cha mpito kuelekea mustakbala unaostahiki.ni azimio linalopokonya Marekani mamlaka ya kipekee nchini Irak iliokua nayo kuweza kujiamua ipendavyo na itakavyo.

Isitoshe, kutangaza kufilisika Marekani na siasa zake nchini Irak ni fursa mpya kwa UM.Na fursa hii inapasa iitumie." Hilo lilikua Kölnerstadt-Anzeiger.

Tofauti kabisa linachambua gazeti la JUNGE WELT kutoka Berlin:

Laandika,

"Azimio la UM kuhalalisha utawala ulioikalia kijeshi Irak lafaa kutafsiriwa ni fanikio la utawala wa Marekani pekee.Hata ukipigiwa debe ni zao la muafaka uliofikiwa kati ya Washington na Paris-Berlin na Moscow ambazo zilikua na tofauti juu ya Irak.

Mamlaka ya nguvu za kijeshi ilizonazo Marekani nchini Irak azimio hilo halibadili kitu.UM ambao haukuidhinisha matokeo ya vita vya Irak vilivyokiuka sheria za kimataifa kuja sasa kuhalalisha ni kujiharamisha binafsi kuwa si halali." Kwa maoni hayo ya JUNGE WELT kutoka Berlin ndio tunageuza sasa mada na kutupia macho soko la ndani la kazi nchini Ujerumani.

Soko la kazi la Ujerumani halioneshi mabadiliko katika hali ya kuselelea ukosefu mkubwa wa kazi humu nchini:Hatahivyo, gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND linaona matumaini: Laandika kwamba,

Kuongezeka ukosefu wa kazi kunapungua ,kwani kwa mara ya kwanza tangu kupita muda mrefu idadi ya nafasi za kazi nayo yaongezeka na sio tu ile ya wasio na kazi.Kwa wanasiasa sasa ile dawa mujarabu ya zamani yafaa kutumika tena-usifanye chochote kinachoweza kuleta dhara.Na hasa haja ya kufufua matumizi masokoni isikandamizwe bali ipaliliwe.Katika hali ya sasa hakuhitaji hatua mpya za kupunguza kodi.....Pale soko la kazi likianza kustawi,ndipo wakati utawadia kuchukua hatua kama hizo za kupunguza matumaizi au kuongeza malipo ya ada au kupandisha riba na Banki Kuu ya Ulaya.

Gazeti la HANDELSBLATT la kibiashara linalochapishwa Düsseldorf linadai kuipitishwa mageuzi yaliodaiwa muda mrefu kufanywa.Laandika,

"Badala kila kukicha kutafuta silaha mpya ya kupambana na ukosefu wa kazi ,serikali ya ujerumani ingepaswa itekelezea mageuzi yaliopendekezwa na halmashauri ya mabingwa maalumu kuhusu soko la kazi.Miongoni mwa mageuzi hayo hasa ni kuregeza masharti ya kuwafukuza wafanyikazi makazini.Ni baada ya kuregeza kamba hizo na kuleta mashari yanayofaa ya kutia raslimali nchini,ndipo uchumi wa ujerumani nao utafufuka na kuanza tena kuimarika.Na hilo ndilo sharti litakalopelekea viwanda kutafuta wafanyikazi.Na hapo tena wanunuzi nao watakua na imani ya kutumia badala ya kuigeuza kila centi upande na huu na ule wakisitasita kutumia."

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW