1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baa la njaa ni nini? Wataalamu wa afya wafafanua

27 Agosti 2025

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Kimataifa linaloangazia mizozo ya chakula, The Integrated Food Security Phase Classification, IPC, imesema ni dhahiri sasa Mji wa Gaza unakabiliwa na baa la njaa. Je, hii ina maana gani?

Palestina Gaza, 2025 | Ukosefu wa chakula
Wapalestina wamekuwa wakitatizika kupata chakula kutokana na kuzingirwa na Israel na mashambulizi yanayoendelea kwenye Ukanda wa Gaza. Hapa wanasubiri kwenye foleni kupokea chakula cha moto kinachosambazwa na shirika la kutoa misaada huko Gaza City, Gaza Julai 16, 2025.Picha: Ahmed Jihad Ibrahim Al-arini/Anadolu/picture alliance

Ripoti hiyo ya IPC iliyochapishwa Ijumaa iliyopita imesema zaidi ya watu nusu milioni huko Gaza sio tu wamenaswa kwenye baa la njaa, bali pia wanakabiliwa na mateso yatokanayo na kukosa chakula na vifo vinavyoweza kuzuilika. 

Hii ni mara ya kwanza kwa IPC kuthibitisha baa la njaa katika eneo hilo la Mashariki ya Kati, ambalo linashambuliwa na Israel inayodai kupigana na kundi la Hamas, tangu lilipofanya shambulizi nchini mwake, Oktoba 7, 2023.

Ripoti hiyo imesema watu wa Gaza wanatagemea kwa kiasi kikubwa misaada kutoka nje kwa sababu hakuna tena uwezo wa kuzalisha kufuatia mashambulizi ya jeshi la Israel, IDF.

Dr. Mark Manary, mtaalamu wa maradhi ya utapiamlo kwa watoto wa tawi la chuo kikuu cha Washington huko St. Louis, amesema ni vigumu kuamini kwamba katika kipindi kama hiki cha mwaka 2025, kuna watu walioko kwenye sayari ya dunia wanaokabiliwa na njaa. Akasema, hakika hicho ni kiashiria cha tahadhari.

Dr. Manary amesema ikiwa chakula kilikuwa kikipatikana kote huko Gaza, itachukua kama miezi miwili ama mitatu kwa eneo hilo kurudi katika hali hiyo

Wapalestina wakisubiri kupokea chakula kutoka shirika la misaada huku kukiwa na janga la njaa, katika Jiji la Gaza, Agosti 18, 2025.Picha: Omar Ashtawy/SIPA/picture alliance

Alisema "Usipopata chakula cha kutosha mwili wako kwanza hutumia hifadhi iliyopo. Kwa hivyo, wote huwa tunaishi kwa sukari ambayo tumeihifadhi angalau kwa siku tatu, na sote tuna mafuta ambayo pia hubakia kwa miezi kadhaa. Kisha mwili utahitaji kuendelea kujilisha kutoka ndani. Kwa hivyo huanza kula misuli yake na baadae aina yoyote ya mafuta. Na athari zinazidi kuongezeka na hatimaye mtu anakufa."

Baa la njaa ni nini?

Dr. Manary anasema kwa lugha rahisi, njaa ni kukosa chakula cha kutosha.

IPC, huthibitisha kuna eneo fulani lina njaa ikiwa mambo haya matatu yatatokea: Kwanza ni ikiwa asilimia 20 ya kaya zitakosa chakula kwa kiasi kikubwa, au kimsingi zina njaa. Pili ni kama angalau asilimia 30 ya watoto watakuwa na utapiamlo mkali au kudhoofika, ikimaanisha kuwa ni wembamba sana ikilinganishwa na urefu wao; na tatu, watu wazima wawili au watoto wanne kwa kila watu 10,000 kufa kila siku kwa njaa na athari zinazosababishwa na hali hiyo.

Mwaka uliopita, wataalamu walitangaza janga la njaa katika maeneo ya Darfur Kaskazini mwa Sudan, Somalia, mwaka 2011 na Sudan Kusini pia ilishuhudia njaa mwaka 2017 ambapo maelfu ya watu waliathirika.

Watoto wa Palestina wakiwa wanapambania chakula kilichogawiwa kwa wakimbizi wa ndani kutokana na mashambulizi ya jeshi la Israel na kujihifadhi Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Hani Alshaer/Anadolu/picture alliance

Nani anatangaza baa la njaa?

Jibu fupi ni kwamba, hakuna kanuni iliyowekwa. Wakati IPC inasema ni "utaratibu wa msingi" unaotumiwa na jumuiya ya kimataifa kuchanganua taarifa na kuhitimisha kama kuna njaa au inakadiriwa njaa inatokea, kwa kawaida haitoi tamko kama hilo wenyewe, ila mara nyingi, maafisa wa Umoja wa Mataifa au serikali watatoa taarifa rasmi, kulingana na uchambuzi kutoka IPC.

Huko Gaza, Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO lilisema utapiamlo miongoni mwa watoto "unaongezeka kwa kasi kikubwa," huku zaidi ya watoto 12,000 wakitambuliwa kuwa na utapiamlo uliokithiri kulipofanyika tathmini mwezi Julai. Hiyo ndiyo idadi ya juu zaidi ya kila mwezi kuwahi kurekodiwa.

Nini hutokea ikiwa wataanza kula?

Ikiwa watu wataanza kula, Dr. Manary amesema hatari yao ya kufa hupungua kidogo katika kipindi cha wiki moja tu. Lakini wakati mwingine huchukua miezi kadhaa kwa mtu kupona kabisa. Wakati baa la njaa linatangazwa, serikali na jumuiya ya kimataifa inayotoa misaada, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa wanaweza kufikisha misaada na ufadhili ili kuwezesha watu wengi zaidi kupata chakula.

Kulingana na ripoti hii ya IPC, kwa kuwa baa hili la njaa limesababishwa na binadamu, linaweza pia kuzuiwa na kuibadilisha hali. Imesema wakati wa kujiulizauliza umepita, baa la njaa lipo na linaenea kwa kasi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW