1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Kamala Harris aanza kampeni za Urais

22 Julai 2024

Chama cha Democratic kimeanza mbio za kuteua mgombea wake kwenye uchaguzi wa Novemba baada ya Rais Joe Biden kujiondoa. Biden amempendekeza makamu wake Kamala Harris kupambana na Donald Trump wa Republican.

Marekani | Kamala Harris | Uapisho wa Makamu wa Rais, 2021
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris akiwapungia mkono raia wakati wa hafla ya uapisho mwaka 2021Picha: Rob Carr/Getty Images

Chama cha Democratic nchini Marekani kimeanza mbio za kuteua atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi ujao mwezi Novemba baada ya Rais Joe Biden kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho jana Jumapili na kumpendekeza makamu wake Kamala Harris kupambana na Donald Trump wa Republican.

Mengi yameendelea kuzungumzwa kufuatia hatua hiyo ya Biden, ambaye alikabiliwa na shinikizo kubwa hivi karibuni la kujiengua kutokana na wasiwasi uliozidi kuhusiana na uwezo wake wa kuongoza.

Mgombea wa chama cha Republican na aliyetarajiwa kupambana na Biden kwenye uchaguzi wa Novemba, Donald Trump, alikuwa miongoni mwa viongozi wa mwanzo kutoa maoni yao kufuatia hatua hiyo. Trump aliandika kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba Joe Biden "hakupaswa kugombea" muhula wa pili. Hakuachia hapo, bali pia alihoji uwezo wake katika muda uliosalia. Biden amesema, ingawa anajitoa lakini bado atabakia White House hadi mwishoni mwa uongozi wake Januari 20, 2025.

Soma pia:Biden aapa kushinda pamoja na kushinikizwa asishiriki uchaguzi wa Novemba 

Wabunge na wazee wa chama hicho, ikwia ni pamoja na karibu theluthi ya maseneta, magavana wenye ushawishi wametoa matamko yao kufuatia hatua hiyo.

Rais Joe Biden na Makamu wake Kamala Harris katika kampeni za urais huko Philadelphia 2024.Picha: Andrew Harnik/Getty Images

Obama, Pelosi wajizuia kuzungumzia uteuzi wa Harris

Bill Clinton, Rais wa zamani wa Marekani pamoja na mkewe Hillary, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya kigeni chini ya Rais Barrack Obama, wamekwishatangaza kumuunga mkono Kamala Harris.

Lakini, majina makubwa kuanzia kiongozi wa walio wachache bungeni Hakeem Jeffries, Spika aliyemaliza muda wake na mwenye ushawishi mkubwa Nancy Pelosi, hadi kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer na Rais wa zamani Barack Obama, wamejaribu kujizuia kusema lolote kuhusiana na hatua hiyo ya kumuidhinisha Harris, ingawa walimpongeza Biden kwa kujiengua.

Soma pia: Shinikizo la kumtaka Biden kutowania muhula wa pili laongezeka

Taarifa ya Obama ilisema tu kwamba watafuatilia mwenendo katika siku zijazo, na kuongeza kuwa ana imani kubwa kwamba viongozi wa chama chake cha Democratic wataweza kuanzisha mchakato utakaoibua mgombea imara.

Soma pia:Trump: Nagombea kuwa Rais wa Marekani yote 

Donald Trump anayewania urais kupitia chama cha Republican katika uchaguzi wa mwezi Novemba, amaehidi kuwa rais wa kila mmojaPicha: Carlos Osorio/AP Photo/picture alliance

Harris aanza kampeni mara moja

Harris, hakuchelewa kuanzisha kampeni ya urais mara baada ya kuidhinishwa na Biden akiwaomba Wademocrats wenzake kumuunga mkono. Maafisa kwenye kampeni yake walianza mara moja kuwapigia simu wajumbe wa mkutano huo mkuu wa chama mwezi ujao wakijaribu kuwashawishi kumuunga mkono mwanamama huyo ambaye huenda akawa wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya Marekani.

Shirika la habari la Reuters liliripoti likinukuu vyanzo mbalimbali kwamba wenyeviti wote 50 wa majimbo wa chama hicho watamuunga mkono Harris. 

Duru zenye uelewa na suala hilo zimesema, Harris, alizungumza na Gavana wa Pennysilvania Josh Shapiro, ambaye huenda akawa mgombea mwenza, kiongozi wa chama hicho bungeni Hakeem Jeffries pamoja na mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Weusi, Steven Horsford.

Kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer, aliyeusifu uamuzi wa Biden wa kuachia ngazi pia hakusema chochote kuhusiana na mgombea ajaye wa chama hicho. Seneta wa kwanza wa Democrats kuanza kumtaka Biden kujiuzulu, Peter Welch yeye alitoa tu wito wa uwazi katika mchakato wa kumpata mgombea.

Mgombea atakayechukua nafasi hiyo ya Biden anatarajiwa kutangazwa katika mkutano mkuu wa Democrats mnamo Agosti 19.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW