Rais Macky Sall aridhia uamuzi wa baraza la katiba
20 Februari 2024Nchini Senegal sakata la kuakhirishwa uchaguzi linaendelea kufukuta,mashirika ya kiraia nchini humo sasa yanataka uchaguzi ufanyike kabla ya muhula wa rais Macky Sall haujakamilika mwezi Aprili. Kwa upande mwingine wagombea 15 wa urais kati ya 20 wanataka uchaguzi huo ufanyike Aprili 2 na sio baada ya hapo.
Rais Macky Sall bado anakabiliwa na shinikizo kutoka kila upande kuhusu hatua yake ya kuakhirisha uchaguzi uliokuwa umepangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu wa Februari.Jana Jumatatu wagombea 15 walisaini barua inayotaka tarehe ya uchaguzi na tarehe ya rais Macky Sall Kuachia ngazi zisipindukie Aprili tarehe 2.
Barua hiyo imeonekana na shirika la habari la AFP na imethibitishwa.Rais Macky Sall ameshasema kwamba dhamira yake ni kuheshimu uamuzi wa baraza la katiba na atafanya mashauriano yanayohitajika kuandaa uchaguzi huo wa raia mapema iwezekanavyo.
Kufuatia siku kadhaa za maandamano nchini humo serikali yake imeamuwa kuwaachilia huru wafungwa 300 katika kipindi cha saa 48 zilizopita. Wengi walioachiliwa ni watu waliokuwa wamezuiliwa jela baada ya kukamatwa na vikosi vya usalama wakati wa maandamano.
Marufuku ya maandamano
Mamlaka za nchi hiyo ziliyapiga marufuku maandamano huku zikifanyika operesheni maalum za jeshi la polisi na kukamatwa kwa wanaharakati wa upinzani. Senegal sio tu iliyazuia maandamano lakini pia ilizima huduma zote za mawasiliano kwa njia ya mtandao.Hata hivyo hivi sasa inaonesha wasenegal taratibu wanataka kuitetea haki yao hiyo ya kuandamana na kuzungumza ambapo yalianza kushuhudiwa maandamano yaliyoruhusiwa kwenye mitaa ya mji wa Dakar na miji mingine mwishoni mwa juma.
Mwanaharakati wa masuala ya kiraia Nina Penda ameiambia Dw kwamba ameshusha pumzi kutokana na hatua mpya za kisiasa zinazochukuliwa akisema kwamba anafurahi sana kuona wafungwa wa kisiasa wamerudishiwa tena uhuru wao. Lakini pia Mwanaharakati huyo amezungumzia juu ya kughadhabishwa kwake kuona ni kwa jinsi gani raia wa Senegal walivyokamatwa kiholela bila ya sababu na maafisa wa polisi walioamuwa kupuuza haki za wananchi.Maamuzi ya baraza la katiba
Itakumbukwa kwamba mnamo Februari 3 rais Macky Sall alitangaza hatua ya kuakhirisha uchaguzi na kuchochea maandamano katika nchi hiyo ambayo waangalizi wengi wakiitazama kama taifa lenye uthabiti wa kidemokrasia.
Maamuzi ya barala la Katiba
Wiki iliyopita baraza la Katiba likaitangaza hatua hiyo ya rais kuwa batili lakini pia kwa upande mwingine majaji wa baraza hilo wakapitisha uamuzi kwamba tarehe ya Desemba 15 iliyotangazwa kama siku ya uchaguzi mpya wa bunge nayo inakwenda kinyume cha sheria na sio halali.
Na mashinikizo hayo ndiyo yaliyomfanya rais Macky Sall kutoa tamko akisema kwamba yuko tayari sasa kufuata maamuzi hayo yaliyotolewa na anataka kuitisha uchaguzi haraka iwezekanavyo.
Tangu uchaguzi ulipoakhirishwa hakuna harakati zozote za kampeini zinazofanyika nchini humo na wanasiasa wengi wa upinzani wamekamatwa kufuatia maandamano.Sambamba na hayo inaelezwa mashauriano kati ya rais huyo anayemaliza muda wake na wagombea 20 wa kiti cha rais yanatajwa kugubikwa na maslahi ya kisiasa ya pande mbali mbali.