1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya sokomoko Ubelgiji, EU kusaini mkataba na Canada

30 Oktoba 2016

Baada ya sokomoko kubwa ambamo mkoa mdogo nchini Ubelgiji ulitishia kuzamisha makubaliano makubwa ya kibiashara yaliojadiliwa kwa miaka saba, hatimaye Umoja wa Ulaya na Canada zinasaini makubaliano hayo ya CETA Jumapili.

Flaggen von Kanada und der EU
Picha: picture alliance/dpa/M. Gambarini

Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau alikubali dakika za mwisho kwenda mjini Brussels kutia saini makubaliano hayo ya kihistoria wakati wa mkutano wa kilele pamoja na rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk na mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claud Juncker.

Awali hafla hiyo ilipangwa kufanyika siku ya Alhamisi lakini ilicheleweshwa baada ya mkoa wa Ubelgiji unaozungumza Kifaransa wa Wallonia, wenye wakaazi milioni 3.6 tu, kukataa kukubaliana na masharti ya makubaliano hayo yanayowaathiri raia milioni 500 wa Ulaya pamoja na Canada.

Mkoa jasiri wa Wallonia ulipinga shinikizo kubwa kutoka pande zote hadi ulipopata muafaka -- kwa maslahi ya kilimo ya kimkoa na uhakikisho kwamba wawekezaji wa kimataifa hawatoweza kuzilaazimisha serikali kubadili sheria -- na hivyo kuiruhusu Ubelgiji kutia saini makubaliano hayo Ijumaa usiku, na kuwawezesha Tusk na Trudeau kupanga tarehe mpya.

Ishara nzuri katika ulimwengu wa mashaka

Sokomoko la Ubelgiji lilipelekea kutolewa onyo kali kuhusu uaminifu wa Umoja wa Ulaya kufuatia kura ya kushtukiza ya Uingereza kujiondoa katika umoja huo, na kwa mfumo mzima wa kiuchumi wa magharibi katika wakati ambapo mashaka makubwa yametawala. Tredeau alisifu hatua hiyo kama "ishara nzuri katika ulimwengu wa mashaka," katika mazungumzo ya simu na Tusk, chanzo kutoka Umoja wa Ulaya kililiambia shirika la habari la AFP.

Kamishna wa Biashara wa EU Cecilia Malmstrom, waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Didier Reynders na balozi wa Canada nchini Ubelgiji Olivier Nicoloff katika hafla ya kutia saini makubaliano ya CETA mjini Brussels Jumamosi Oktoba 29, 2016.Picha: picture-alliance/dpa/N. Maeterlinck

Akitilia mkazo ahueni iliopatikana kwa uande wa Umoja wa Ulaya, ambao unapambana kubakia pamoja katika wakati ambapo Ulaya inakabiliwa na mgogoro wa wakimbizi uliyosababishwa na vita nchini Syria na kuhusiana na sera yake kuelekea Urusi, waziri mkuu huyo wa zamani wa Poland Tusk alitwiti kwamba "Kazi imekamilika!"

Waziri wa mambo ya nje wa Ubelgiji Didier Reynders alisema "hakuna kilicho rahisi nchini Ubelgiji lakini ni mambo machache sana ndiyo hayawezekani" wakati akitia saini rasmi makubaliano hayo siku ya Jumamosi.

Makubaliano hayo hayo ambayo yanajulikana rasmi kama "Comprehensive Economic and Trade Agreement (CETA), yanaondoa asilimia 99 ya ushuru wa forodha kati ya pande mbili, na kuliunganisha soko la pamoja na Umoja wa Ulaya lenye watu 500, na Canada - taifa la kumi kwa uchumi mkubwa duniani na mwanachama wa kundi la matafa saba yalioendelea zaidi kiviwanda G7.

Lakini makubaliano hayo yaliingia mashakani kutokana na maandamano kutoka Wallonia -- mkoa uliosheheni kwa viwanda katika kanda ya kusini ya Ubelgiji, ambao kwa sasa umetelekezwa na viwanda vyake kuota kutu, pamoja na upinzani kutoka kwa jamii za watu wanaozungumza Kifaransa.

Makubaliano hayo yanayahitaji mataifa yote 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuyaridhia na katika baadhi ya matukio -- kama ilivyotokea kwa Ubelgiji -- serikali za mikoa pia zinahitaji pia kutoa idhini yake, hii ikimaanisha kuwa mkoa wa Wallonia na mingine ilikuwa inazuwia makubaliano hayo kwa ufanisi.

'Hakuna hata nukta iliyobadilishwa'

Waziri mkuu wa Ubelgiji Charles Michel alifanya mazungumzo ya muda mrefu katika juhudi za kuishawishi mikoa, na hatimaye kutangaza siku ya Alhamisi kwamba pande mbili zimefikia makubaliano, yanayowezesha mataifa mengine 27 kuridhia makubaliano hayo.

Michel alisisitiza kuwa mazungumzo marefu ya Wallonia hayakubadilisha hata nukta katika katika makubaliano. Lakini Paul Magnette, kiongozi wa serikali ya mkoa wa Wallonia na mwakilishi wa wapinzani wa CETA, alisema alipata uhakikisho kutoka serikali ya shirikisho kuhusu ulinzi imara wa kijamii na kimazingira.

Waandamanaji wakiwa na bango lenye maneno yasemayo,"raia milioni 3.4 wa Ulaya wanaitegemea Wallonia - Sitisheni CETA" waakti mkutano kuhusu CETA ukiendelea katika bunge la Wallonia mjini Namur, Ubelgiji Oktoba 18, 2016.Picha: GettyImages/AFP/N. Lambert

Baada ya kugonga mwamba katika mazungumzo na viongozi wa Wallonia wiki iliyopita, waziri wa biashara wa Canada ailezungumza kwa hisia, Chrystia Freeland, alikaribia kulia wakati akiutaja Umoja wa Ulaya kama jumuiya isiyo na uwezo wa kupata makubaliano ya kimataifa.

Mkataba wa Umoja wa Ulaya na Canada pia umevutia upinzani mkubwa kutoka kwa wanaharakati wanaopinga utandawazi wa kampeni ya "Zuwia CETA" wanaosema unadhoofisha viwanda vya ndani na viwango vya huduma za afya na mambo mengine.

Pia katika makubaliano hayo wanaona njama kubwa zaidi na tata ya makubaliano kati ya Umoja wa Ulaya na Marekani. Majadiliano ya makubaliano hayo - maarufu kama Transatlantic Trade and Investment Partnership (TTIP), yamekwama katika wiki za karibuni, ambapo lengo la kuyaidhinisha kufikia mwishoni mwa muhula wa rais Barack Obama limewekwa kando.

Matatizo ya mkataba wa Canada hata hivyo yameonekana kama kielelezo cha mambo magumu yanayoweza kutokea kwa Uingereza wakati ikijaribu kujadili mkataba mpya wa biashara na Umoja wa Ulaya baada ya kuondoka katika kanda hiyo -- yumkini mwaka 2019.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe

Mhariri: Isaac Gamba