1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baadhi ya Warusi wataka kuukana uraia wao

Admin.WagnerD23 Machi 2022

Athari ya vita vya Ukraine inazidi kuonekana huku baadhi ya raia wa Urusi waliokimbilia katika mataifa ya ulaya, sasa wanapiga hatua nyingine ya kutaka kuukana uraia wao.

Russland I Ukraine-Konflikt - Proteste in St. Petersburg
Picha: Dmitri Lovetsky/AP/picture alliance

Roman Sukhanov ni raia wa Urusi ambaye anaishi katika mji wa mwambao wa magharibi nchini Sweden wa Gothernburg. Sukhanov alifika hapa miaka kumi iliyopita kama mkimbizi wa Urusi, miaka miwili baada ya kuikimbia  nchi yake Rais Putin aliliteka eneo la Crimea lililoko katika mwambao wa kaskazini wa bahari nyeusi mashariki mwa ulaya na kulifanya kuwa sehemu ya Urusi

Sasa Urusi inapigana vita nchini Ukraine. Roman Sukhanov anasema hii inatosha na ameamua kuchukua hatua zaidi ya kuukana uraia wake wa Urusi na kuwa raia wa Sweden kwa kubadili majina na kuliacha jina lake la kirusi. ''Sababu sitaki kuhusishwa na Rais Putin na vitendo vyake vya uharifu wa kivita na ndiyo maana nimeamua kuanza mchakato wa kulibadili jina langu na kuachana na uraia wangu wa mwanzo na kujipanga na uraia mpya.Kwa sababu miaka iliyopita warusi wote walihusisha na vita na vitendo vibaya, na safari hii nina wasiwasi kwamba ninaweza kuwa kwenye shutuma zinazofanywa na nchi yangu za kufanya mauaji na kupoteza maisha ya watu wasio na hatia.'' Anasema Sukhanov.

Waandamanaji wa Urusi walipambana na polisi Moscow kupinga uvamizi wa UkrainePicha: Sergei Fadeichev/TASS/dpa/picture alliance

Sweden ni moja ya nchi zinazoendelea kupokea wakimbizi wa Urusi na Ukraine kupitia nchi jirani za Norway, Denmark na Poland. Wiki iliyopita lilifanyika tamasha la wanamuziki maarufu nchini Sweden kwa ajili ya kukusanya pesa za msaada kwa wakimbizi wanaoingia, wakati huo zilitolewa shuhuda mbalimbali za kile kinachoendelea nchini Ukraine. ''Kuanzia jana najaribu kupiga simu ili kuzungumza na ndugu zangu niliowaacha Ukraine lakini simu haipiti inawezekana wamepata matatizo au pengine simu imeisha umeme...kwa sababu hali ni ngumu hakuna maji hakuna umeme wala chakula.'' Alisema mkimbizi mmoja. 

Soma pia: Urusi yaongeza mashambulizi katika miji ya Ukraine

Kwake Sukhanov anasema hakuitegemea hali hii kutokea huku lawama zote akizielekeza kwa Rais Putin wa Urusi

"Ni uhalifu mbaya wa kivita na ni vigumu kuamini na si kwangu pekee isipokuwa kwa warusi wote ambao wanaendelea kuwa na aibu kila pande za dunia.Mama yangu anaishi Marekani lakini nusura moyo wake usitishe mapiga alipopata taarifa ya kuanza mapigano haya. Rais Putin anataka kurejesha eneo la shirikisho la zamani la Urusi kwa gharama za maisha ya watu wasio na hatia lakini hakika hatofanikiwa.'' Alisema.

Kwa upande mwingine serikali ya Sweden tayari imetangaza asilimia 2%ya pato jumla la nchi hiyo kupelekwa moja kwa moja katika wizara ya ulinzi kutokana na kuimarisha usalama wa nchi hiyo ambayo imeshaonywa na Urusi karibu mara mbili dhidiya kujiunga na shirika la kujihami la nchi za NATO

Sylvanus Karemera, DW, Sweden

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW