Baba Mtakatifu aanza ziara yake Ujerumani
22 Septemba 2011Baba Mtakatifu amesema jamii inaendelea kuwa mbali na Mungu wakati alipowasili mjini Berlin. Kiongozi huyo amekaribishwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais Christian Wulff.
Ziara ya Papa Benedikt XVI nchini Ujerumani haikosi sababu. Hali ya kanisa Katoliki nchini humu ni ngumu. Kufuatia madai ya visa vya udhalilishaji wa kingono waumini wengi wa kanisa Katoliki wanalihama kanisa. Ndio maana kauli mbiu ya ziara yake ni " Alipo Mungu, hapo ndipo kwenye mustakabali wa maisha ya baadaye".
Wajerumani watakiwa wasilikimbie kanisa
Baba Mtakatifu amewahimiza Wajerumani wasilimbie kanisa kutokaba na visa vya unyanyasaji wa kingono.
Amesema ana hamu kubwa ya kukutana na viongozi wa kanisa la Kiinjili la Ujrumani wakati atakapolitembelea kasri la Erfuhrt.
"Hatutarajii msisimko mkubwa, lakini tunataka kwa pamoja tulifikirie eneo hili, tusikie neno la Mungu na tuombe pamoja. Tukaribiane ili tulete umoja wa Wakristo wote."
Kengele za Vatikan zimepigwa wakati papa atakapowasili leo huko Berlin, ikiwa ni mara ya tatu kwa kiongozi huyo. Alishawahi kuhudhuria kongamano la vijana mjini Cologne mnamo mwaka 2005 na kuutembelea mji alikozaliwa huko Bayern. Safari hii anashukia mji mkuu, Berlin, kwa mara ya kwanza kwa ziara rasmi.
Baada ya kufanya mazungumzo na rais Wulff na kansela Merkel, papa Benedikt XVI atalihutubia bunge la Ujerumani, Bundestag, tukio linaloelezwa kuwa kubwa muhimu kwa kiongozi wa kanisa Katoliki. Hilo ni suala linalomfurahisha sana mwenyekiti wa baraza la maaskofu wa kanisa Katoliki hapa Ujerumani, askofu mkuu Robert Zollitsch kutoka mjini Freiburg.
"Tunafurahia kwamba baba mtakatifu anakuja Ujerumani kwa ziara rasmi. Na bila shaka tutamkaribisha kwa moyo mkunjufu."
Ziara ya papa yapingwa
Hata hivyo, Benedikt XVI hakaribishwi na kila mtu. Wabunge takriban 100 wa chama cha upinzani cha Social Democratic, SPD, chama cha walinda mazingira cha Kijani, na cha Die Linke, wanapinga kwa kuwa wanaamini kiongozi wa dini hapaswi kuingia bungeni. Hans-Christian Ströbele, mbunge wa chama cha Kijani mjini Berlin amesema, "Tukianza kuwaenzi viongozi wa makanisa na wa kidini katika bunge la Ujerumani, je hilo linatakiwa kumalizikia wapi?"
Watu takriban 20,000 wanajiandaa kuandamana katika jiji la Berlin kupinga msimamo wa kanisa Katoliki kuhusiana na maadili ya uhusiano wa kimapenzi. Miongoni mwa waandamanaji hao ni Volker Beck, mbunge wa chama cha Kijani, ambaye ni shoga. Anasema linapokuja suala la haki za binadamu na sera kuhusu mapenzi, Baba Mtakatifu hapiganii kile ambacho katiba ya Ujerumani inatarajia kutoka kwa viongozi.
Askofu mkuu Zollitsch kwa upande wake amesema hapingi maandamano ya kuipinga hotuba ya papa Benedikt XVI bungeni. Hata hivyo amesisitiza kwamba kiongozi huyo alialikwa na spika wa bunge la Ujerumani na kuna haja ya kuheshimu maoni ya kila mtu.
Papa anapendwa na wengi
Idadi wa wafuasi wanaomuunga mkono Baba Mtakatifu hapa Ujerumani ni kubwa kuliko wanaompiga. Kwa misa nne za hadhara zitakazofanyika Berlin, Erfuhrt na Freiburg, wamejiandikisha watu 250,000. Uwanja wa mpira wa Berlin, Olimpiastadion, umejaa pomoni, kukiwa hakuna tena tiketi. Watu wanataka kumuona Baba Mtakatifu.
Mwandishi: Riegert, Bernd/Josephat Charo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman