1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba Mtakatifu aomba radhi

Abdu Said Mtullya12 Aprili 2014

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameomba radhi juu ya vitendo vya uovu vilivyofanywa na baadhi ya makasisi wa kikatoliki

Papa Francis
Papa FrancisPicha: Getty Images

Papa Francis amesema anaibeba yeye binafsi lawama juu ya uovu wa kubakwa na kubughudhiwa kingono kwa watoto, na amewaomba radhi waliofanyiwa uovu huo. Amelitaka Kanisa Katoliki liwe na ujasiri mkubwa zaidi katika juhudi za kuwalinda watoto.

Hii ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu kukubali kuibeba lawama yeye mwenyewe binafsi, juu ya uhalifu wa kingono uliotendwa na makasisi, na ameomba msamaha.

Papa atoa ishara thabiti:

Kauli ya Papa Francis, aliyoitoa papo kwa papo ni ishara nyingine inayoonyesha jinsi anavyoutambua uzito wa uovu uliotendwa na makasisi, baada ya kukosolewa na asasi zinazoyatetea maslahi ya watu waliotendewa uhalifu wa kingono na makasisi, kwa kile asasi hizo zilikiona kuwa ni kushindwa kwa kanisa kulipa suala hilo uzito.

Hatua kuchukuliwa dhidi ya wahalifu:

Mabadiliko yalianza mwezi uliopita wakati Baba Mtakatifu alipowateua wanawake wanne na mhanga mmoja wa uhalifu wa kingono kuwa wajumbe wa bodi ya ushauri, ambayo Kanisa Katoliki limesema italishughulikia suala muhimu la adhabu, kwa maaskofu wanaowakingia kifua wanaowafisidi watoto.

Hanna Suchocka, mjumbe wa tume ya kuwalinda watotoPicha: picture-alliance/dpa

"Ni wajibu wangu kuibeba lawama", Baba Mtakatifu aliyasema hayo kwa wawakilishi wa mtandao wa mashirika ya kikatoliki ya nchini Ufaransa yanayozilinda haki za watoto.

Papa Francis alikutana na wawakilishi hao kwenye maktaba yake ya Vatican. Aliwaambia "nahisi ninao wajibu wa kuibeba lawama mimi binafsi juu ya ouvu wote uliotendwa na makasisi wengi na naomba radhi".

Baba Mtakatifu amesema kuwa Kanisa Katoliki linayatambua madhara yaliyofanyika. Ameeleza kuwa Kanisa Katoliki halitarudi nyuma katika hatua za kulishughulikia tatizo hilo na ametamka kwamba adhabu zitatolewa. Ameeleza kwamba badala ya kurudi nyuma, Kanisa litapaswa kuwa na nguvu zaidi. Amesema watu wasiyachezee maisha ya watoto.

Papa aunda tume ya ushauri:

Mwezi uliopita, Baba Mtakatifu aliwateua wajumbe wa tume wa kumshauri juu ya njia za ufanisi za kupambana na uhalifu wa kingono unaotendwa na makasisi. Nusu ya wajumbe wa tume hiyo ni wanawake, mmoja wao akiwa Marie Collins aliefanyiwa ufidhuli na kasisi, alipokuwa mtoto. Collins ambae baadae alikuja kuwa mwanaharakati maarufu wa kutetea haki za walionyanyaswa kingono alitoa mwito kwa Papa wa hapo awali, Benedikt, kumtaka aombe radhi juu kashfa iliyofanyika na juu ya viongozi wa Kanisa walioweka utiifu wao kwa kanisa mbele, kabla ya usalama wa watoto.

Marie CollinsPicha: Filippo Monteforte/AFP/Getty Images

Kanisa Katoliki limesema tume hiyo sasa itaziweka kanuni na kuyaangalia majukumu ya kisheria na wajibu wa watumishi wa kanisa, kwa maana kwamba, watalishughulikia suala muhimu la kuwachukulia hatua maaskofu waliosaidia kuuficha uhalifu.

Wahanga wataka hatua zaidi:

Asasi muhimu ya wahanga wa ufidhuli ya nchini Marekani "SNAP" imesema kuwa inataka kuziona hatua zaidi zikichuliwa. Wawakilishi wa asasi hiyo wamesema wanaitaka dunia ijali zaidi vitendo kuliko maneno. Mkurugenzi wa asasi hiyo amesema kabla Baba Mtakatifu hajachukua hatua thabiti kwa ajili ya kuwalinda watoto, dunia itakuwa na haki ya kuwa na mashaka na vile vile itapaswa iwe macho.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Ape
Mhariri: Grace Patricia Kabogo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW