1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba Mtakatifu asaidia Haiti.

Erasto Mbwana28 Septemba 2004

Mafuriko ya maji yaliyosababishwa na kimbunga cha Jeanne yameua zaidi ya watu 2,000 katika mji wa Gonaives ulioko kaskazini mwa Haiti. Waokoaji bado wanaendelea kupata maiti nyingi siku kumi baada ya kimbunga hicho kukivamia kisiwa hicho. Watu 1,000 wametangazwa rasmi kuwa wamepotea na wengine 300,000 hawana maskani.

Maafisa wa serikali, mashirika ya kimataifa ya misaada na Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaleta misaada ya dharura kisiwani Haiti. Lakini ingawaje ni hivyo, magenge ya Wanaume wenye mitarimbo wameshambulia misafara ya malori ya vyakula yanayowasili Gonaives.

Meya wa mji wa Gonaives, Calixte Valentin, amesema, "Hatuna idadi kamili ya watu waliofariki lakini tunaamini kuwa idadi hiyo ni kubwa kuliko ile iliyotolewa na Mamlaka ya Ulinzi wa Raia."

Mji huo wenye Wakazi kati ya Laki mbili na Laki mbili na nusu umevurugwa kabisa na kimbunga hicho. Mamia ya wakazi wake sasa wanahifadhiwa kwa muda ndani ya Kanisa Kuu la Gonaives wakati Maafisa wa Afya wana wasiwasi kuwa huenda magonjwa ya matumbo na kuharisha damu yakazuka.

Meya Valentin amesema kuwa maiti nyingine 50 zimepatikana katika wilaya ya Dolan na kuzikwa katika makuburi ya pamoja.

Meya mstahiki amesema, "Makaburi kumi yamechimbwa kwa ajili ya maiti zilizopatikana masaa machache yaliyopita ndani ya vifusi vya nyumba zilizo haribiwa chini ya matope mengi na kando kando ya pwani ambako zilikuwa zikielea."

Valentin amekosoa kile alichokiita ukosefu mkubwa wa ulinzi na nidhamu katika ugawaji wa chakula kinachohitajiwa sana pamoja na misaada mingine ya lazima.

Majeshi ya kimataifa ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yamepewa jukumu la kulinda vituo muhimu vya ugawaji wa chakula na kuzuia kuvamiwa na Wahaiti wenye njaa.

Wanajeshi hao wamefyatua risasi za maonyo hewani na kufyatua pia gesi za kutoa machozi mwishoni mwa juma kwa lengo la kuutawanya Umma uliotishia kuvivamia baadhi ya vituo vya vyakula.

Waziri Mkuu wa mpito wa Haiti, Gerard Latortue, amezungumzia uwezekano wa kuwahamisha kwa muda wakazi wa Gonaives.

Amesema, "Tunachunguza uwezekano wa kuwahamisha baadhi ya wakazi hadi katika maeneo jirani kwa lengo la kusafisha na kupulizia madawa nyumbani ili kuzuia magonjwa."

Hospitali kuu ya Gonaives nayo pia imekumbwa na mafuriko yaliyosababisha Wagonjwa mia kadhaa wasiojiweza kuuawa.

Nchi za Amerika na Ulaya zimeahidi kutoa fedha za dharura na kusafirisha kwa meli tani kadhaa za misaada ya vyakula na dawa.

Vatikani imetangaza kuwa Baba Mtakatifu Yohana Paulo II ameamuru Dollar Laki moja zitolewe kwa lengo la kuwasaidia Wahanga wa mafuriko hayo.

Fedha hizo zitatumiwa kwa kununulia maji ya kunywa, vyakula na dawa kwa ajili ya Wahanga wa kimbunga cha Jeanne kilichoikumba nchi hiyo Septemba 18. Kimbunga hicho kimeivuruga pia Jamhuri ya karibu ya Dominiki na Puerto Rico.

Serikali ya Colombia imetangaza kuwa inapeleka tani 25 za vyakula na dawa kisiwani Haiti na Grenada ambayo imekumbwa na kimbunga kinachoitwa Ivan.

Misaada hiyo itapelekwa kwa ndege ya mizigo ya Jeshi la Angani la Colombia baadaye leo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Amerika, Miguel Angel Rodriguez, ameziomba nchi zote za Umoja huo kuisaidia Haiti.

Bw. Rodriguez, akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Shirika la Afya la Panamerican (PAHO) mjini Gonaives, amesema, "Changamoto yetu ni kubwa kisiwani Haiti. Lazima tuwasaidie wakazi wake na kile kilichotokea katika taifa hili la Karibiki ni changamoto kubwa kwa uadilifu wetu wa kijamii."

Haiti imewahi kukumbuwa na kimbunga kingine kilichosababisha watu kadhaa kuuawa mwezi wa Mei mwaka huu hali kadhalika na vita vibaya vya kikabila mwanzoni mwa mwaka huu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW