Baba Mtakatifu azungumza na maaskofu.
17 Februari 2010Baba Mtakatifu Benedikt wa 16 amelaani uhalifu wa kuwalawiti watoto wa kiume makanisani kuwa ni dhambi dhidi ya mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu ametoa shutuma hizo baada ya kukutana na maaskofu kwenye makao yake makuu ya Vatican.
Kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani ametoa kauli hiyo kufuatia kufichuka kwa habari juu ya ufidhuli uliotendwa na makasisi nchini Ireland wa kuwalawiti watoto. Baba Mtakatifu Benedikt wa16 amesema pamoja na kuwa vitendo vya kuchukiza, ufidhuli huo ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu amelaani kudhalilishwa kwa watoto wa kiume kingono kuwa siyo tu ni uhalifu, bali pia ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu.
Amesema vitendo hivyo vinakiuka hadhi ya mwanadamu alieumbwa kwa mfano wa Mungu.
Baba Mtakatifu amewataka maaskofu wa Ireland aliokutana nao kwa muda wa siku mbili wachukue hatua ili kurejesha imani na uadilifu wa kanisa.
Kanisa katoliki nchini Ireland lilikumbwa na kashfa ya watoto wa kiume kugeuzwa wanawake baada ya tume iliyoongozwa na hakimu Ynonne Murphy kulishutumu kanisa katoliki nchini Ireland kwa kutoyazingatia ipasavyo madai juu ya kutendeka kwa mikasa 300 ambapo watoto wa kiume walilawitiwa.
Tume hiyo ilitoa lawama hizo mwezi novemba mwaka jana kuhusiana na madai ya kufanyika vitendo hivyo katika dayosisi ya Dublin kati ya mwaka 1975 na 2004.
Makasisi 24 wa Ireland walioitwa na baba Mtakatifu kujadili kashfa hiyo walimwambia kiongozi huyo wa kanisa katoliki kuwa wametahayari juu ya kashfa hiyo na wameahidi kushirikiana na kanisa.
Katika tamko lao maaskofu hao wamesema hatua muhimu sasa zimechukuliwa ili kuhakikisha usalama wa watoto na vijana watakaohusiana na shughuli za kanisa.
Mwandishi Mtullya/ZA AFPE
Mhariri: Miraji Othman