1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba wa mshambuliaji wa bomu Manchester akamatwa

Sekione Kitojo
25 Mei 2017

Uingereza taratibu imeanza  kukaribia kupata taarifa sahihi  za mtandao  wa  kundi la jihadi  linalofikiriwa  kuhusika na shambulio katika  ukumbi wa tamasha la muziki mjini Manchester

Schweigeminute - Manchester
Waombolezaji wakiweka mauaji katika eneo la tukio mjini ManchesterPicha: Reuters/S. Wermuth

Wakati  maombolezo  yaliyochanganyika  na  hasira  kuhusiana  na  kuvuja kwa  taarifa  nchini  Marekani  zinazohusiana  na  uchunguzi  wa tukio  hilo yakiendelea, taarifa  zinasema  baba  yake mshambuliaji Salman Abedi  alikuwa  mmoja  wa  wanamgambo  wa  kundi  la itikadi  kali  lenye  mafungamano  na  al-Qaeda.

Nchi  ya  Uingereza  ambayo  ilikumbwa  na  mshituko  baada  ya shambulio  hilo  la  kigaidi , ilitulia  kwa  muda  wa  dakika  moja kuanzia  saa  tano  asubuhi  saa  za  Uingereza kuwakumbuka  watu 22  waliofariki  katika  shambulio  hilo, wahanga  ambao  hawana hatia  katika  shambulio  la  hivi  karibuni  kabisa  lililodaiwa  na kundi  la  Dola  la  Kiislamu  kwamba  wao  ndio  walifanya shambulizi hilo.

Waombolezaji mjini ManchesterPicha: picture-alliance/PA Wire/B. Birchall

Na  wakati  majina  zaidi  ya  watoto yakitajwa  miongoni  mwa wahanga  wa  mauaji  ya  siku  ya  Jumatatu, maafisa  nchini  Libya walimkamata  baba  wa  mshambuliaji  huyo  pamoja  na  kaka  yake wakati  polisi  nchini  Uingereza  walifanya  msako  mwingine na kuwakamata  watu wengine.

Watu zaidi wakamatwa

Baba  yake  Abedi, Ramadan , "alikuwa  mmoja  wa  wanamgambo wa  kundi  la  Libyan Islamic Fighting Group LIFG," amesema  Ahmed bin Salem , msemaji  wa  majeshi ya  Libya, ambayo  yanachukua nafasi  ya  polisi  katika  serikali ya  umoja  wa  kitaifa  nchini  Libya.

Malkia Elizabeth wa pili akitembelea hospitali walikolazwa majeruhi wa shambulio hilo mjini ManchesterPicha: picture alliance/empics/P. Byrne

Ramadan Abedi  alikuwa  akisakwa  na  utawala  wa  kiongozi  wa zamani  wa  Libya  Muammar Gaddafi  kwa  mahusiano  yake na kundi lililopata  ukimbizi  Uingereza  kabla  ya  kurejea  nchini  Libya mwaka  2011  na  kujiunga  na  vuguvugu  la  mapinduzi  yaliyokuwa yakiungwa na  NATO  ambayo  hatimaye  yaliuondoa  utawala  wa Gaddafi.

Kundi  hilo  ambalo  hivi  sasa  limevunjwa  lilianzishwa  mwaka 1995  na  Walibya  ambao  walipigana  na  majeshi  ya  iliyokuwa Umoja  wa  Kisovieti  nchini  Afghanistan na  kuendelea  kubakia huko  baada  ya  majeshi  hayo  kujiondoa.

Lengo pekee  la  kundi  hilo  lilikuwa  kuuondoa  utawala  wa Gaddafi.

Mshambuliaji  huyo  wa  kujitoa  muhanga Salman Abedi  huenda alitengeneza  mwenyewe  bomu  alililoliripua  ama  alipata  msaada fulani  kutoka  kwa  mshirika  wake, duru zenye vyanzo karibu  na uchunguzi  zimeliambia  shirika  la  habari  la  Reuters. Polisi wamesema  leo  wamewakamata  watu  muhimu  na  kugundua  vitu muhimu  wakati  wakichunguza  shambulio  hilo  la  bomu  mjini Manchester.

Polisi wakilinda doria mjini Manchester baada ya shambulioPicha: Getty Images/L. Neal

Polisi  ya  Manchester  inawashikilia  kwa  sasa  watu  wanane, baada  ya  kumwachia  huru  mwanamke leo  bila  ya  kumfungulia mashitaka.  Taarifa  zinasema  pia  kwamba  mshambuliaji  huyo alisimama  kwa  muda  katika  uwanja  wa  ndege  wa  Istanbul  kabla ya  kwenda  kufanya  shambulio  hilo.

Serikali ya  Marekani kuchukua  hatua

Wakati  huo  huo mwanadiplomasia  mwandamizi  zaidi  wa Marekani  nchini  Uingereza  Lewis Lukens , ameshutumu uvujishaji wa  taarifa  kwa  vyombo  vya  habari, akisema  serikali  ya Marekani  itachukua  hatua  kuwataja  wale  waliohusika. Mchambuzi wa  masuala  ya  usalama na afisa wa zamani  wa  ujasusi Bob Ayers  amesema  hali  hiyo  itafikia  mwisho  hivi  karibuni.

"Mara  ya  mwisho  nilipoangalia  polisi  ya  manchester haikuzungumza  kwa  niaba  ya  Uingereza, haizungumzi kwa mikataba  ya  kimataifa, kwa  hiyo polisi ya  Manchester huenda ikakasirishwa lakini yatakwisha."

Na nchini  Uingereza  polisi  wenye  silaha  wanafanya  doria  katika treni  nchini humo kuanzia  leo  kwa  mara  ya  kwanza , polisi inaohusika  na  masuala  ya  usafiri imesema , baada  ya  kiwango cha hofu ya  ugaidi  kupandishwa  kuwa hali  mbaya  kufuatia shambulio  mjini  Manchester.

Kbabu ya soka ya Manchester United pamoja na majirani zao wa Manchester City wameahidi kutoka Pauni milioni 1 kwa mfuko wa dharura wa shambulioPicha: picture-alliance/ZUMA Wire/Xinhua/Gong Bing

Navyo vilabu viwili  maarufu  mjini  Manchester , United  na  City vimechangia  kiasi  ya pauni  milioni  moja  katika  mfuko  wa dharura ulioundwa baada  ya  shambulio  katika  mji  huo.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / rtre / afpe

Mhariri: Yusuf , Saumu

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW