1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Bachelet akosolewa kwa ziara ya China

29 Mei 2022

Marekani imeungana na makundi ya haki za binaadamu kuonesha wasiwasi wao kwamba ziara ya Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa nchini China haikuleta faida yoyote kwa hali ya haki za binaadamu.

Treffen zwischen Präsident Xi Jinping und Michelle Bachelet
Picha: United Nations High Commissioner for Human Rights/AP/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya mambo ya kigeni ya Marekani siku ya Jumapili (Mei 28) ilisema nchi hiyo inatiwa wasiwasi sana "na ziara ya Michelle Bachelet na kikosi chake nchini China na juhudi za China kuibana na kuipotosha ziara hiyo."

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Anthony Blinken, alisema masharti yaliyowekwa na mamlaka za China "hayakuruhusu kufanyika tathmini huru na kamilifu ya mazingira ya haki za binaadamu, ikiwemo kwenye jimbo la kaskazini magharibi la Xinjiang, ambako matendo ya mauaji ya maangamizi na uhalifu dhidi ya ubinaadamu yanaendelea."

Washington ilikuwa imeonya kabla ya Bachelet kufanya ziara yake ya muda mrefu nchini China kwamba mamlaka za huko zisingelimpa fursa itakayomuwezesha kuwa na tathmini kamili ya hali ya haki za binaadamu.

Kwenye taarifa yake ya Jumamosi, Blinken alirejelea msimamo huo, akisema "amekerwa na ripoti kwamba wakaazi wa Xinjiang walitishwa kwamba kamwe wasilalamike wala kuzungumzia kwa uwazi hali wanayokabiliana nayo na wala hakukutolewa taarifa yoyote juu ya walipo mamia ya watu wa jamii ya Uighur waliopotea wala hali za mamilioni ya watu wanaoshikiliwa."

Bachelet atetea ziara ya China

Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, (kushoto) na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Wang Yi.Picha: Deng Hua/IMAGO

Akizungumza kwenye mkutano wake wa mwisho na waandishi wa habari mjini Guangzhou, Bachelet alisema kwamba hakuwa amekwenda China kwa kufanya "uchunguzi bali alikuwa ameitwa na serikali ya China kuhakiki hatua zake za kupambana na ugaidi kuhakikisha kwamba zinakidhi viwango vya kimataifa vya haki za binaadamu."

Kwenye mazungumzo yake, alijiepusha kuikosowa moja kwa moja serikali ya China baada ya ziara yake iliyojumuisha miji ya Kashgar na Urumqi katika mkoa wa Xinjiang. 

Shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch lilisema mkuu huyo wa haki za binaadamu "anaonekana kuamini kuwa ana nguvu kubwa za ushawishi kiasi cha kwamba mazungumzo yake ya chumbani yataishawishi Beijing kulegeza ukandamizaji."

"Lakini Beijing itazungumza kwa furaha kwenye vikao vya faragha hadi uso wake utamemetuka kwa furaha. Itajibu tu kukiwa na shinikizo la umma," alisema mkurugenzi wa shirika hilo, Kenneth Roth, kupitia ukurasa wa Twitter.

Baraza la Uyghur lamkosowa Bachelet

Polisi wakimkamata mwanamke wa Uighur nje ya ubalozi wa China mjini Ankara, Uturuki.Picha: Burhan Ozbilici/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa Baraza la Uyghur Duniani, ambalo linawakilisha makundi ya watu wa jamii hiyo wanaoishi uhamishoni, "ziara hiyo imegeuka kuwa propaganda kwa ajili ya China kusafisha uhalifu wake dhidi ya ubinaadamu na mauaji ya maangamizi dhidi ya watu wa jamii ya Uyghur."

Hii ilikuwa ziara ya kwanza ya mkuu wa kamisheni ya haki za binaadamu nchini China ndani ya miaka 17, ambayo ilitanguliwa na mawasiliano ya kina kati ya Bachelet na Beijing. 

Ziara hii ilifanyika baada ya kuchapishwa ugunduzi mpya kutokana na data zilizovujishwa kuonesha kiwango cha ukatili na mateso kwenye mkoa wa Xinjiang. 

Serikali ya China inawatuhumu Waislamu wa jamii ya Uighur katika mkoa huo kwa kusambaza fikra za kujitenga, siasa kali na vitendo vya kigaidi. 

Waislamu walio wachache nchini China wanasema wanakabiliwa na ukandamizaji wa kisiasa, kidini na kitamaduni. 

Ujerumani ilisema data hizo mpya zinaonesha "ushahidi mpya wa uvunjaji mkubwa wa haki za binaadamu" nchini China.