Bachelet Mkuu Mpya Baraza la Haki za Binadamu-UN
10 Agosti 2018Wajumbe walio wengi katika Baraza kuu la Umoja wa mataifa wamepiga kura za ndiyo kumuidhinisha Bibi Bachelet baada ya hapo jana Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress kuwasilisha pendekezo la kumteua Rais huyo wa Zamani wa Chile kuongoza moja ya vyombo muhimu ndani ya Umoja wa Mataifa
Bachelet anachukua nafasi ya Zeid Al-Hussein, mwanadiplomasia kutoka Jordan ambaye muhula wake wa miaka minne kama mkuu wa chombo hicho unamalizika mwishoni mwa mwezi Agosti.
Uongozi wa mtangulizi wake ulikabiliwa na kizungumkuti hali iliyopelekea Zeid Al-Hussein kufutilia mbali mipango ya kuwania muhula wa pili baada ya kupoteza uungwaji mkono wa mataifa yenye nguvu ikiwemo China, Urusi na Marekani.
Zeid mara kadhaa alizikasirisha nchi zenye nguvu kutokana na kuzikosoa waziwazi kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kutokana na mwenendo wa Zeid makundi ya haki za binadamu yalikuwa na wasiwasi kuwa Gutteres angemteua mtu asiye mzungumzaji sana kuchukua wadhifa huo muhimu.
Michelle Bachelet ni Nani?
Bachelet mtoto wa jenerali wa zamani wa jeshi la anga la Chile ana historia ya kusisimua ikiwemo kuwahi kuzuiliwa kwa wiki kadhaa mwaka 1975 kwenye kambi moja ya mateso mjini Santiago baada ya baba yake kupinga mapinduzi yaliyofanywa na Dikteta Augusto Pinochet dhidi ya serikali ya Salvador Allende.
Mkuu wa Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch amesema historia ya Bachelet ya kuwa mhanga wa ukiukwaji wa haki dhidi yake inaleta mtizamo mpya ndani ya tume ya haki za binadamu katika wajibu wake wa kulinda kikamilifu haki za binadamu ulimwenguni.
Bachelet alichaguliwa mnamo 2006 kuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini Chile na baada ya muhula mmoja mwaka 2010 aliteuliwa kuongoza Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake.
Mwaka 2013 alirejea Chile ambapo aliwania na kushinda muhula mwingine madarakani uliomalizika miezi michache iliyopita.
Kuhusu Bachelet, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Halley ambaye nchi yake ilitangaza kujiondoa kutoka Baraza la Haki za Binadamu mwezi juni amesema mkuu huyo mpya atapaswa kujiepusha na makosa ya nyuma ya kuilenga zaidi Israel kwenye kazi zake na kupuuza ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika maeneo mengine duniani.
Ofisi ya Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu ambayo Bachelet ataiongoza inaratibu juhudi za Umoja wa Mataifa katika kulinda na kuhimiza haki za binadamu pamoja na kupaza sauti dhidi ya ukiukwaji wake kote ulimwenguni.
Mwandishi: Rashid Chilumba/APE/AFP
Mhariri: Josephat Charo