1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado kuna changamoto ya kuudhibiti Ugonjwa wa kifua kikuu

24 Machi 2021

Ulimwenguni unapoadhimisha Siku ya Kupambana na ugonjwa wa Kifua Kikuu hii leo, bado kuna changamoto nyingi zinazokabili hatua za kuudhibiti na hadi kuutokomeza ugonjwa huu.

Tuberkolose in Südafrika
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Schermbrucker

Maradhi ya Kifua Kikuu huenda yakawa janga ikizingatiwa usimulizi wa anayeugua au aliyewahi kuugua, ambao wengi wanakumbana na tatizo la unyanyapaa. Maureen Otieno, afisa wa zahanati katika hospitali ya Madianyi – Rarieda jimboni Siaya na ambaye amewahi kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu anasema jamii imechangia wagonjwa wengi kujificha wengi wakihofia kuhusishwa na maradhi ya Ukimwi.

Jimboni Kisumu, idadi kubwa ya wagonjwa wa Kifua Kikuu wanapatikana katika maeneo ya vitongoji duni.

Afisa Msimamizi Mkuu, kitengo cha matibabu na maradhi ya Kifua Kikuu, jimboni Kisumu Timothy Malika, anasema ugonjwa huo unaathiri na kusambaa kwa kasi miongoni mwa watu wanaoishi katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu hii ikiwa ndio hali katika maeneo ya vitongoji.

Daktari, Beatrice Okwaro Okoo, mratibu wa matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, eneo bunge la Kisumu ya Kati amesema juhudi za kutoa matibabu kwa waathiriwa wa ugonjwa huo unachangiwa na watu wengi kutojitokeza kutafuta matibabu hospitalini kwa kuhofia vipimo huenda vitadhihirisha maradhi zaidi ya Kifua Kikuu.

Usisitishe matibabu unapopata nafuu

Picha: Getty Images/M. Safodien

Hatua ya wagonjwa wengi kusitisha matibabu pindi wanapopata nafuu pia ni kikwazo kikubwa katika kukabiliana na Kifua Kikuu na ni hatari zaidi kwa usalama wa mgonjwa maana huishia kwa maradhi haya kujenga kinga dhidi ya matibabu.

soma zaidi: WHO: Kifua kikuu ndiyo ugonjwa hatari zaidi wa maambukizi

Kwa mujibu wa zoezi la kutoa matibabu dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu unaoendeshwa na Mpango wa Komesha Kifua Kikuu, Mpango wa Kitaifa wa Kifua Kikuu, kwa ushirikiano na serikali za majimbo ya Kisumu, Siaya na Homabay, takwimu za wiki moja zimerekodi maambukizi 14 Kisumu, 26 Siaya na 29 Homabay chini ya kauli mbiu yenye msisitizo wa ugonjwa wa Kifua Kikuu, una Tiba.

Kadhalika, takwimu za Mpango wa kitaifa wa Ugonjwa wa Kifua Kikuu, ugonjwa wa Ukoma na mardhi ya mapafu NTLD nchini Kenya, kati ya wagonjwa 100,000 wanaotafuta huduma za matibabu hospitalini, 426 wanaugua Kifua Kikuu, asilimia 64 wakiwa ni wanaume na asilimia 36 wanawake huku pakiwa na hofu kuwa takwimu nyengine hazinakiliwi.

Mwandishi: Musa Navie