1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado May hajamalizana na Brexit

26 Novemba 2018

Wakati akiwa amefanikisha kupata ridhaa ya viongozi wenzake wa Umoja wa Ulaya juu ya kujiondoa kwa nchi yake kwenye Umoja huo, ukweli ni kwamba bado siasa za ndani ya Uingereza hazimkalia sawa Waziri Mkuu Theresa May.

EU-Sondergipfel zum Brexit in Brüssel
Picha: Reuters/D. Martinez

Mnamo tarehe 23 Juni 2016, wakati wa kura ya maoni, wapiga kura milioni 17.4 , au asilimia 52, waliunga mkono mpango huo wa Brexit, huku watu milioni 16.1 au asilimia 43 wakipiga kura kusalia katika umoja huo. Lakini tangu siku hiyo, wanaopinga wamekuwa wakitafuta mbinu za kuandaa kura nyingine ya maoni.

May mara kwa mara amesema kwamba hakutaitishwa kura nyingine ya maoni na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Jeremy Corbyn pia ameashiria kuwa haungi mkono pendekezo hilo. Je, ni njia gani itatumika kwa kura nyingine ya maoni kuandaliwa?

Kwanza, kulingana na wanaoendesha kampeni, ni kwa bunge kukataa rasimu ya mpango huo wa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya. Ili kujiondoa katika Umoja huo kulingana na masharti ya mapngo wake, May atahitaji uungaji mkono wa Bunge. 

Hata hivyo, idadi ya wanompinga katika chama chake cha Conservative na hasira ya wenzake katika Chama cha Demokrasia cha Ireland Kaskazini inaonesha kuwa atakuwa na wakati mgumu kupitisha mpango wake, licha ya kuwa na uungaji mkono wa wabunge wa chama cha Labour.

Kuangushwa kwa mpango wa May kutaiweka Uingereza katika matatizo makubwa. Mawaziri wakuu watatu wa Uingereza miongoni mwa wanne walio hai - John Major, Tony Blair na Gordon Brown, wamesema awamu ya pili ya kura ya maoni ndio njia pekee ya kutatua mgogoro uliopo.

Mwezi uliopita, Blair aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba kuna uwezekano wa mpango wa Brexit kusitishwa.

Ugumu bungeni

Chama cha upinzani cha Labour, ambacho pia kimegawanyika kutokana na suala la Brexit, kimeashiria kutafuta njia ya kufanikisha uchaguzi mwingine iwapo May atashindwa kupata uungaji mkono wa Bunge. Lakini ili uchaguzi mwingine uandaliwe, thuluthi mbili ya wabunge 650 wanafaa kupiga kura ya kuungan mkono.

Picha: Getty Images/Bloomberg/J. Juinen

Njia nyingine ni iwapo kura ya kutokuwa na imani na serikali itapitishwa. Kisha kutakuwepo na muda wa wiki mbili kupitisha sheria ya kuwa na imani na serikali mpya.

Iwapo hakutakuwepo na kura ya kutokuwa na imani na serikali hiyo mpya, uchaguzi mpya lazima uandaliwe katika muda wa siku 17. Waendesha kampeni wa Brexit wanadhani kuwa chama cha Labour kitashindwa kufanikiwa kuwezesha uchaguzi mwingine kufanywa.

Baada ya kile kitakachokuwa wiki kadhaa za mgogoro na kushindwa kwa njia nyingine kama vile uchaguzi, waziri mkuu mpya, jaribio la kufanya majadiliano tena na Umoja wa Ulaya, Bunge hatimaye litaitisha kura nyingine ya maoni.

Utaratibu halisi haujawekwa wazi lakini wabunge huenda wakapiga kura kwa hoja itakayoitisha kura ya maoni ikiwa njia moja ya kujiondoa katika msuguano. Hilo lazima liungwe mkono na sheria kwa wito wa kura ya maoni.

Ikumbukwe kuandaliwa kwa kura ya maoni kutachukua miezi kadhaa na Umoja wa Ulaya utaitishwa muda zaidi wakati Uingereza inapojiandaa kujiondoa katika Umoja huo tarehe 29 Machi 2019.

Majaji katika Mahakama ya Juu zaidi ya Umoja wa Ulaya watasikiliza kesi kuhusu mchakato wa Brexit tarehe 27 mwezi huu wa Novemba, kutathmini iwapo Uingereza inaweza kubadili uamuzi wake wa kujiondoa katika Umoja huo.

Wanaounga mkono Brexit wanasema kuandaliwa kwa kura nyingine ya maoni kutaitumbukiza Uingereza katika mgogoro mkubwa zaidi wa kikatiba kuwahi kushuhudiwa, na hata kusababisha vurugu. 

Mwandishi: Sophia Chinyezi/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman
 
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW