Baerbock aionya Ulaya kuhusu mvutano wa China na Taiwan
13 Aprili 2023Akizungumza katika ziara yake ya China, Baerbock ameonekana kutoa matamshi tofauti na yale ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wiki iliyopita alipoutaka Umoja wa Ulaya "usijihusishe na mizozo isiyo yake" alipokuwa akilizungumzia suala la Taiwan. Matamshi hayo ya Macron yalikosolewa pakubwa na Marekani na mataifa ya Ulaya.
Nchi za Umoja wa Ulaya zinatarajia kwamba Ujerumani itaitumia fursa ya ziara hiyo ya kwanza ya waziri wake wa mambo ya nje China, kuuweka wazi msimamo wa Umoja wa Ulaya kwa China.
Soma pia: Ujerumani yatoa wito wa kupunguzwa kwa mivutano ya China na Taiwan
Hata bila kauli hiyo ya Macron, ziara ya Baerbock ilikuwa inatazamwa kwa karibu kwa kuwa waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani amekuwa mkosoaji mkubwa wa China hata kumshinda Kansela Olaf Scholz, kwani kwa sasa anataka kuwasilisha bungeni sera ya Ujerumani kwa China, ambapo anataka kupunguza kiwango cha biashara Ujerumani inachofanya na China.