Baerbock ataka mageuzi katika Umoja wa Mataifa
2 Juni 2026
Baerbock amesema hakuna mbadala wa Umoja wa Mataifa kwani ndio jukwaa pekee lenye sauti sawa kwa nchi zote 193. Hata hivyo, amekiri kuwa jitihada za mageuzi hukwamishwa na migogoro ya kisiasa.
Baerbockamezihimiza nchi kuheshimu sheria za kimataifa akionya kuwa kushindwa kufanya hivyo kunadhoofisha umoja huo.
Kauli zake zinajiri kabla ya kura kuhusu ombi la Ujerumani kupata kiti katika Baraza la Usalama. Amesema chombo hicho kina jukumu muhimu la kulinda amani duniani.
Amesema pia Baraza la Usalama linapaswa kuhakikisha wanachama wote wanazingatia sheria za kimataifa, ikiwemo wale wa kudumu wenye haki ya turufu.
Baerbock ameonya kuwa migogoro ya kisiasa na mvutano wa kijiografia vinaifanya kazi ya Umoja wa Mataifa kuwa ngumu zaidi kuliko hapo awali.
Ameongeza kuwa dunia inakabiliwa na hatari nyingi zinazohitaji ushirikiano wa karibu wa kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda misingi ya umoja huo.
Kwa mujibu wake, bila ujasiri wa nchi wanachama kushikamana na kanuni za pamoja, mfumo wa kimataifa unaweza kudhoofika zaidi.