Baerbock ziarani Mashariki ya Kati mwishoni mwa juma
5 Januari 2024Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Sebastian Fischer aliuambia mkutano wa kawaida na waandishi wa habari siku ya Ijumaa kwamba Baerbock atafanya mazungumzo na waziri mpya wa mambo ya nje wa Israel, Israel Katz, pamoja na Rais Isaac Herzog.
Pia atakutana na rais wa mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas na waziri wa mambo ya nje Riyad al-Maliki.
Baerbock baadaye atasafiri kwenda Misri kukutana na waziri mwenzake Sameh Shoukry na pia alipanga kuzuru Lebanon.
Soma hapa: Ujerumani yahimiza uwajibikaji wa kimataifa katika ukanda wa Gaza
Mazungumzo hayo yatazingatia "hali ya kushutusha ya kibinadamu huko Gaza, hali ya Ukingo wa Magharibi na hali tete katika mpaka wa Israel na Lebanon", pamoja na juhudi za kuachiliwa kwa mateka zaidi wa Hamas.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Baerbock alisema kwamba Waisraeli na Wapalestina "wataweza tu kuishi bega kwa bega kwa amani ikiwa usalama wa mmoja unamaanisha usalama wa mwingine".
Hofu imezidi kutanda kuwa huenda mzozo kati ya Israel na Hamas ukaenea baada ya mmoja wa viongozi wa kundi hilo la wanamgambo kuuawa katika viunga vya Beirut.
Soma kuhusu taarifa hii: Baerbock: Ujerumani inatumai Israel itazuia madhila kwa Wapalestina
Mbali ya mauaji hayo ambayo yanadhaniwa kuwa yamefanywa na Israel, jeshi la Israel limekuwa kwa miezi kadhaa katika makabiliano ya risasi kwenye mpaka na wanamgambo wa Hezbollah.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken pia alianza ziara yake siku ya Alhamisi huko Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na Israel, naye pia kiwa ni ziara yake ya nne tangu vita kuanza.