1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baerbock ziarani China

Hawa Bihoga
13 Aprili 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock anaanza ziara yake nchini China leo Alkhamisi ambapo mbali na mambo mengi analenga kuweka sera ya pamoja ya Umoja wa Ulaya kuhusu Beijing.

MSC - Münchener Sicherheitskonferez |  Annalena Baerbock
Picha: ODD ANDERSEN/AFP/Getty Images

Katika ziara hiyo ya siku mbili Baerbock anatawajiwa kukutana na mwenyeji wake Qin Gang pamoja na mwanadiplomasia mkuu wa China Wang Yi.

Ajenda ambazo zinapewa kipaumbele katika ziara hiyo ni pamoja na kuikumbusha China jukumu lake la kuishawishi Urusi kumaliza uvamizi wake nchini Ukraine, na kusisitiza msimamo wa Ulaya kuhusu hali mambo katika Mlango wa Bahari Taiwan haikubaliki.

Mtazamo wa Ulaya kuhusu China kama mshirika ,mshindani na mpinzani wa kimfumo ni miongoni mwa dira na sera za Umoja huo.

Soma pia:China yaendeleza luteka za kijeshi kuizunguka Taiwan

Msemaji wa  Wizara ya Mambo ya Nje Ujerumani  Andrea Sasse, amesema wasiwasi ni mkubwa kuhusu hali ya mambo huko Taiwan na hivyo ni jukumu la kila upande ikiwa ni pamoja na China kuchangia katika kuleta utulivu na amani.

"Tunatoa wito kwa washirika wote katika kanda,kuzuia kutetereka kwa hali ya utulivu katika mlango wa bahari wa Taiwan." Alisema

Ameongeza kuwa Berlin inatumia njia zote za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo katika ngazi mbalimbali.

Macron: EU Tupunguze utegemezi kwa Marekani

Ziara ya Baerbock inafanyika katika wakati ambapo bado kuna fukuto kwa washirika wa Ulaya na Marekani baada ya matamshi yenye mkanganyiko yaliotolewa na Raisi wa Ufaransa Emmanuel Macron.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron Picha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Katika mahojiano na moja ya chombo cha habari nchini Ufaransa Macron amesema, Umoja wa Ulaya unapaswa kupunguza "utegemezi" kwa Marekani.

Soma pia:Taiwan yapuuza vitisho vya China

Macron ambae hivi karibuni alikuwa ziarani nchini China akiambatana na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, alionya dhidi ya kutumbukizwa kwenye mzozo kuhusu Taiwan unaoendeshwa kwa muelekeao wa Marekani na majibu "Makali" ya China.

"Nasisitiza umuhimu wa kujitegemea kimkakati kati ya washirika haimaanishi kuwa kibaraka."

Alisema kiongozi huyo huku akisisitiza kuwa ni wakati kwa mataifa ya Umoja wa Ulayakukumbuka kwamba kila mmoja kwa nafasi yake bado anayo haki ya kufikiri peke yake kama nchi.

Wachambuzi:Kauli ya Macron ni ushindi kwa Beijing

Wanasiasa wengi wa Ulaya,wanadiplomasia na wachambuzi wanaitazama kauli ya Macron ni kama ushindi kwa Beijing kwa kile walichokiita lengo la kusambaratisha umoja kati ya Ulaya na washirika wake.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na mwenzake wa China Xi JinpingPicha: Ng Han Guan/AP/picture alliance

Lakini wachambuzi wanasema, matokeo yake nia ya safari ya Bearbock imeongezeka huku wananchama wengi wa Umoja wa Ulaya wakitumai Berlin itatumia mwanya huo kuweka wazi msimamo wao wa pamoja dhidi ya China.

Soma pia:China yasema itachukua hatua iwapo Rais wa Taiwan atakutana na Spika wa Bunge la Marekani

Mbali na siasa Baerbock amesema anatarajia kuzungumzia fursa za ushirikiano zaidi kati ya China na Ulaya katika kukuza jumuiya za kiraia, kupambana na mabadiliko ya hali ya hewana katika sekta nyingine zinazoinukia katika dunia ya sasa ya teknolojia kama vile nishati mbadala.