BAGHDAD :Viongozi wanaolani Al Qaeda hadharani washambuliwa
12 Agosti 2007Viongozi wawili wa KiSunni nchini Iraq wanaopinga vitendo vya ugaidi wa Al Qaeda hadharani walishambuliwa katika visa viwili tofauti.Shambulio hilo linaashiria kuwa mtandao huo wa ugaidi huenda ukashambulia viongozi wowote wanaoupinga.Wakati huohuo bomu moja la kutegwa barabarani limesababisha kifo cha gavana mmoja na mkuu wa polisi kwenye eneo la kusini linalozongwa na mapigano makali kati ya makundi ya Kishia yanayozozana.Waziri Mkuu wa OIraq anatoa wito wa kutulia bila kulipiza kisasi.
Mashambulizo hayo yanaelezea namna Iraq inakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wapiganaji wa Kishia na waSunni walio na misimamo mikali.Marekani kwa upande wake inaunga mkono muungano wa viongozi wa Kisunni unaopinga shughuli za kundi la Al Qaeda.Hata hivyo mashambulizi hayo yanaelezea jinsi viongozi hao wanakabiliwa na tishio endapo wanajiunga na muungano huo.
Katika kisa kimoja wapiganaji walishambulia kwa bomu nyumba ya kiongozi wa kidini wa KiSunni aliye na msimamo wa wastani Sheik Wathiq al -Obeidi aliyepinga vitendo vya Al Qaeda hivi karibuni.
Sheikh Wathiq alijeruhiwa vibaya sana na jamaa zake 3 kuuawa.Kundi la wanamgambo wa Kisunni lilimtahadharisha Kiongozi huyo mwanzoni mwa juma lililopita na kumueleza kuwa msaliti na kumlaumu kwa kushirikiana na baraza la viongozi wa kitamaduni wa KiSunni linaloungwa mkono na Marekani.Baraza hilo linapambana na ugaidi magharibi mwa Iraq.