1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Watu 60 wauwawa nchini Iraq

12 Desemba 2006

Mshambuliaji wa kujitolea muhanga maisha amejiripuwa na kuuwa watu 60 na kujeruhiwa wengine kadhaa katikati ya Baghdad leo hii baada ya kuushawishi umma wa watu wanaotafuta kazi za vibaruwa kwenda kwenye gari lake kwa ahadi ya kuwapatia kazi.

Polisi imesema watu zaidi 150 wamejeruhiwa wakati gari lake hilo liliporipuka saa moja asubuhi katika Uwanja wa Tayran.Milio ya risasi ilisikika mara tu baada ya mripuko huo.

Uwanja wa Tayran ni sehemu mahsusi ya mkusanyiko wa maseremala.mafundi bomba,wafyatuaji wa matofali,wapaka rangi na wafanyakazi wengine za vibaruwa katika biashara ya ujenzi ambao huzurura kwenye mikahawa na kufanya uchuuzi wakati wa asubuhi wakisubiri nafasi ya kupatiwa kazi.

Kutokana na kuendelea kwa umwagaji damu nchini Iraq Rais George W. Bush wa Marekani amezitaka nchi jirani na Iraq kusaidia kuinusuru serikali ya nchi hiyo.Wito wake huo unaonekana kuwa ujumbe usio wa moja kwa moja kwa Syria na Iran.

Bush leo anatarajiwa kuzungumza kwa njia ya video na makamanda wa kijeshi wa Marekani walioko Baghdad na hapo kesho atakutana na Makamo wa Rais wa Iraq Tariq al Hashemi.