1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bajeti ya DRC, masuala ya kijamii yapewa kipaumbele

Saleh Mwanamilongo, DW Kinshasa.19 Novemba 2019

Katika bajeti yake ya kwanza serikali ya Rais Felix Tshisekedi imetenga asilimia 30.1 kwa ajili ya masuala ya kijamii. Elimu imetengewa asilimia 21, Afya imetengewa asilimia 6 na 0.3 kwa ajili ya malipo ya uzeeni.

DR Kongo Felix Tshisekedi beim Kinshasa Digital Forum
Picha: Präsidentschaft der DR Kongo/G. Kusema

Bajeti ya kwanza ya serikali ya Rais Felix Tshisekedi nchini Kongo imesomwa bungeni leo ambako asilimia 20 ya bajeti hiyo imetengwa kwa ajili ya sekta ya elimu. Bajeti ya mwaka 2020 imefikia dola bilioni 10 ya matarajio. Upinzani hata hivyo umeikosoa bajeti hiyo ukisema imesheni uongo mtupu na serikali haina uwezo wa kukusanya fedha hizo.

Akiupigia debe bungeni mswaada huo wa bajeti, waziri mkuu Sylvestre Ilunga, amesema kwamba asilimia 30 ya bajeti hiyo zinatengwa kwa ajili ya maswala ya jamii.

"Tunatilia maanani gharama za hali ya maisha ya wananchi wetu, huku tukitenga asilimia 30.1 kwa ajili ya masuala ya kijamii. Sekta ya elimu inapewa asilimia 21, sekta ya afya imepewa asilimia 6, na nukta 3 kwa ajili ya malipo ya uzeeni."

Rais Tshisekedi alitangaza kwamba elimu ya msingi ni bure kwa wanafunzi wote nchini, na serikali imetenga asimilia 11 ya bajeti yake kwa ajili ya gharama za shule ya msingi,hata hivyo fedha hizo hazifikii  asilimia 50 ya jumla ya gharama za shule ya msingi kwa mwaka.

Kwa mujibu wa wataalamu ni kwamba ikiwa elimu ya shule ya msingi itatolewa  bure,gharama yake ni dola bilioni 2 nukta tano kwa mwaka.

Upinzani unaelezea kwamba serikali haina uwezo wa kukusanya fedha hizo,kwanza kutokana na uwezo mdogo wa kiuchumi. Kila mwaka bajeti ya serikali inategemea kwa asili mia 90 ushuru na kodi kutoka kwenye sekta yake ya madini. Hasa madini ya shaba na kobolt. Hivi sasa bei ya madini hayo kwenye soko la kimataifa  imezidi kuporomoka.

Bunge la Jamhuri ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya CongoPicha: AFP/Getty Images/J. D. Kannah

Mbunge Henri Thomas Lokondo, anahisi mageuzi yaliotarajiwa kutoka serikali mpya bado ni ndoto

"Wametegemea kukusanya fedha kutokana na kodi na ushuru mwengine,inamaanisha kwamba ni raia ambao watateswa katika kuongezewa mzigo wa kodi kwa hiyo sijuwi wanamaana gani wakisema  watabadilisha hali ya maisha ya raia. Serikali ambayo haizalishi chochote inategemea tuu sekta moja ya madini ambayo siku hizi hayana soko."

Ikiwa wabunge waliowengi ni kutoka chama vyama tawala vya FCC na CACH, lakini wao pia waliohoji  utaratibu utakao tumiwa na serikali katika kukamilisha miradi ya maendeleo. Nadine Mangabu ambaye ni mbunge wa vuguvugu la CACH,la Rais Felix Tshisekedi amesema:

"Kuna kodi inayolipishwa kila mwezi kuhusu kusadia miradi ya vijana lakini kila mwaka tunaposoma bajeti hatuone hamala fedha hizo zimepelekwa. Inaleta wasiwasi kuhusu uwekezaji kwa ajili ya vizaji vijavyo."

Kwenye ripoti iliotolewa na wizara ya fedha kuhusu matumizi ya bajeti ya mwaka uliopita ni kwamba ikulu ya rais ilitumia mara nne zaidi , yaani asilimia mia nne ya bajeti yake. Kwa jumla ni kwamba asimilia 50 ya bajeti imekuwa ikitumiwa kwa ajili ya mishahara na utendaji kazi wa taasisi za serikali.