1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bajeti ya mwaka 2010 magazetini

Oumilkher Hamidou25 Juni 2009

Nakisi ya bajeti inatazamiwa kufura-wanasema wahariri

Waziri wa fedha Peer SteinbrückPicha: AP

Mjadala kuhusu bajeti ya mwaka 2010 na mjadala kuhusu kuwepo vikosi vya Ujerumani nchini Afghanistan ndizo mada zilizohanikiza magazetini hii leo.Tuanzie lakini na mgogoro wa bajeti ambao gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE linasema serikali ya muungano imeshindwa kuupatia ufumbuzi.Gazeti linaendelea kuandika:

Juhudi za kutuliza mfumo wa fedha na kufufua shughuli za kiuchumi,zinahitaji subira hata kama watu watabishana kuhusu kiwango na umuhimu wa misaada hiyo.Kisichoweza kusameheka lakini ni ule uzembe uliofanyika.Tukumbuke kwamba serikali ya muungano wa vyama vikuu iliingia madarakani ikijiwekea shabaha ya kupunguza kwa kiwango kikubwa nakisi ya bajeti-na kupandisha ikilazimika kodi za mapato.Hapo lakini serikali ya muungano imeshindwa,licha ya madaraka makubwa iliyo nayo.

Gazeti la "Sächsische Zeitung" la mjini Dresden linaandika:

"Katika taarifa yake chapwa, Peer Steinbrück hakuficha aliposema hakuna upenu wa kupunguza kodi za mapato kama vyama ndugu vya CDU/CSU vinavyofikiria.Amekwepa lakini kutoa maelezo yoyote yale juu ya namna wanavyofikiria kuboresha hali ya mambo au wapi wanafikiria kupunguza gharama.Anasema kwa tabasamu waziri Steinbrück" angekua mwendawazimu" kama ,muda mfupi kabla ya uchaguzi mkuu,angefichua wapi wanapanga kupunguza matumizi.Kwa maneno mengine na hili ni sawa kwa serikali nzima ya muungano wa vyama vikuu,inamaanisha kwamba ,hawako tayari kuwaambia ukweli wananchi.Ni mbinu za uchaguzi hizo ambazo kwa kweli ni adha tupu."

Gazeti la "Die Tageszeitung la mjini Berlin linaashiria nakisi itazidi kuongezeka.Gazeti linaaendelea kuandika:

Nakisi ya bajeti itaongezeka kupita kiasi mwakani.Inaweza kufikia yuro bilioni 100 .Hali hiyo inamaanisha tutashuhudia kiini macho katika kampeni za uchaguzi.Hakuna si SPD na wala si vyama ndugu vya CDU/CSU,kinachosubutu kutamka,wana mikakati ya aina gani au kodi gani wanapanga kupandisha au hata huduma gani za jamii wanapanga kupunguza.

Mada ya pili magazetini inahusiana na kutumwa wanajeshi wa Ujerumani nchini Afghanistan.Gazeti la "Der neue Tag la Weiden linaandika:

Waziri wa ulinzi Franz Josef Jung (kushoto)Picha: AP

"Wanajeshi wa Ujerumani wanaotetea uhuru nchini Afghanistan,wanafyetuliwa risasi na maguruneti.Wanauwawa wakiwa ndani ya vifaru vyao.Wana jihisi wameingia vitani.Ujerumani ikitaka kuwatuma watoto wake,wake kwa waume katika maeneo yanayodhibitiwa na wataliban,itabidi iwapatie vifaa bora kabisa vya kijeshi kwa namna ambayo wataweza kutambua shida zao zinazingatiwa.

Kuhusu hali nchini Afghanistan,gazeti la "Emder Zeitung linaandika:

Mjadala usiokua na maana yoyote kuhusu Afghanistan umepamba moto mjini Berlin.Watu wanabiashana kama jeshi la shirikisho linahusika na vita au la nchini humo.Waziri wa ulinzi anakana,mjumbe maalum anaeshughulikia masuala ya kijeshi anasema "ndio jeshi la shirikisho linaendesha vita nchini Afghanistan.Ukweli ni kwamba wanajeshi kadhaa wa Ujerumani wameuwawa katika shughuli zao ambazo waziri wa ulinzi anazitaja kua ni za kiutu,na zinazohusiana na mpango wa kuijenga upya Afghanistan.Hicho ni kiini macho.Bila ya shaka wanajikuta vitani wanajeshi wa Ujerumani kwa mfano wanapokutana na watzaliban na baadae kupoteza maisha yao.Hawajaanguka kutoka ngazini walipokua wakijenga shule,badala yake wameuliwa kikatili kabisa.Mjumbe anaeshughulikia masuala ya jeshi,kasema sawa kabisa alipozungumzia hali halisi namna ilivyo."


Mkusanyaji :Oummilkheir Hamidou/ Dt Zeitungen

Mhariri: Abdul-Rahman


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW