1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Bakhmut iko hatarini kuangukia mikononi mwa Urusi

8 Machi 2023

Muungano wa kijeshi wa NATO Jens Stolteberg umeonya kwamba mji wa Bakhmut wa Ukraine ulioharibiwa kwa mashambulizi makali ya hivi karibuni huenda ukaangukia mikononi mwa Urusi katika siku zijazo.

Belgien | NATO | Treffen Jens Stoltenberg mit Dmytro Kuleba und Josep Borrell
Picha: Valeria Mongelli/AFP/Getty Images

Katibu mkuu wa muungano wa kijeshi wa NATO Jens Stolteberg amesema ingawa Urusi imepata pigo kubwa katika mapambano kwenye mji huo, lakini hiyo haimaanishi kwamba mji huo mwishowe hauwezi kuchukuliwa. 

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari huko mjini Stockholm pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya.

Amesema "Na tunachoona ni kwamba Urusi inapeleka wanajeshi zaidi ila wanachokikosa ni ubora. Na wanajaribu kuliziba pengo hilo kwa kuongeza wanajeshi. Wamepata pigo kubwa. Lakini wakati huo huo, hatuwezi kukataa kwamba Bahmut hatimaye itachukuliwa siku zijazo. Naa hii haiakisi kwamba labda kuna mabadiliko yoyote kwenye vita, na hatupaswi kuidharau Urusi. Ni lazima tuendelee kuisaidia Ukraine."

Tangazo hili linatolewa baada ya rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuonya kwamba iwapo Bakhmut itaangukia mikononi mwa Urusi, ni wazi kwamba adui wake huyo atapata mlango mwingine wa kuimarisha mashambulizi zaidi nchini humo. Kiongozi wa kundi la wapiganaji la Wagner la nchini Urusi amedai mapema leo kwamba wamelikamata eneo la mashariki la mji huo wa viwanda wa Bakhmut, ambako kumeshuhudiwa mapigano makali kati ya wanajeshi wa Ukraine na Urusi kwa miezi kadhaa sasa.

Mawaziri hao wa ulinzi wa Ulaya wamekutana Stockholm, kujadiliana mikakati ya kuongeza misaada ya kiulinzi na silaha nchini Ukraine na kulingana na mkuu huyo wa NATO, msaada wa silaha haulingani na kiwango kinachotakiwa na Ukraine kwa sasa, katika wakati ambapo inakabiliwa na mashambulizi ya kila siku na kuwatolea mwito mawaziri hao wa mataifa 21 wanachama wa Umoja wa Ulaya pamoja na NATO kuongeza msaada wa ulinzi ili Ukraine iweze kujilinda na uvamizi wa Urusi.

Pendekezo la kununua silaha kwa pamoja lakumbwa na kizingiti.

Mmoja ya wakazi wa Bakhmut akiwa amesimama karibu na jengo lililoharibiwa na makombora ya Urusi Picha: Alex Babenko/REUTERS

Waziri wa ulinzi wa Ukraine Oleksii Reznikov kwa upande wake amewahimiza mawaziri wenzake wa Ulaya kuunga mkono mkakati wa kununua makombora milioni moja ili kuisaidia Kyiv. Akizungumza na waandishi wa habari akiwa Stockholm, Reznikov amesema Ukraine inahitaji makombora hayo kwa haraka ili kujibu mashambulizi ya kushtukiza ya Urusi.

Reznikov amesema anaunga mkono pendekezo la Estonia kwa niaba ya Umoja wa Ulaya la kuungana ili kununua makombora hayo kwa mwaka huu, yenye thamani ya yuro bilioni 4 akisema wanahitaji kati ya makombora 90,000 hadi 100,000 kwa mwezi.

Lakini mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya Josep Borrell, badala yake alipendekeza mpango ambao ungetumia fedha ambazo zimetengwa kwenye wakfu wa Umoja huo kwa ajili ya masuala ya amani wa European Peace Facility. Na alipoulizwa kuhusu pendekezo hilo la Estonia alisema na hapa namnukuu, "fedha hazianguki kutoka angani", na sio kwa sababu tu kwamba mwanachama mmoja wa Ulaya anadai kwamba tunahitaji fedha zaidi, basi fedha hizo zitatokea kimiujiza." mwisho wa nukuu.

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius, yeye amekubaliana na pendekezo la kuungana kwa ajili ya manunuzi ya makombora hayo akisema hatua hiyo ni muhimu, lakini ni wazi watambue tu ya kwamba itachukua muda kwa viwanda kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji hayo makubwa kwa sasa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW