1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balaa la kimbunga Idai lawatesa Wamsumbiji

19 Machi 2019

Huenda zaidi ya watu 1000 wakawa wameuwawa na kimbunga Idai kilichosababisha mafuriko makubwa katika maeneo mbali mbali ya Msumbiji,mpaka Zimbabwe na Malawi. Hali inatisha zaidi nchini Msumbiji

Mosambik Beira Zyklon Sturm  Idai
Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Onyodi

Nchini Msumbiji kimbunga idai kilichosababisha mafuriko mabaya kabisa kimeendelea kuzusha hofu na wasiwasi. Rais wa nchi hiyo Phillipe Nyusi ameiambia Redio msumbiji kwamba idadi ya waliouwawa kufuatia janga hilo huenda ikafikia mpaka watu 1000.

Rais Phillipe Nyusi alifanya ziara katika maeneo yaliyokumbwa na mafuriko na kimbunga idai akitumia helikopta na kusema kwamba mpaka sasa vifo 84 vimeshathibitishwa ingawa taarifa za waokoaji pamoja na picha zinazoonesha uharibifu kutokea angani zinamfanya kiongozi huyo kuwa na hofu kwamba hadi watu 1000 huenda wameshafariki.

''Kwa sasa tumeandikisha rasmi  vifo vya watu 84 lakini tulipozunguka kwenye eneo lililoathirika asubuhi hii ili kufahamu kilichokuwa kinaendelea,kila kitu kilionesha kwamba kuna uwezekano tukaandisha vifo vya zaidi ya watu 1000. Zaidi ya watu laki moja wako hatarini''

Mashirika ya msaada hata hivyo yameonya , kiwango kamili cha uharibifu uliosababishwa na kimbunga idai pamoja na mafuriko hakiwezi bado kutabirika.

Rais Nyusi  ameeleza jinsi alivyoona maiti za watu zikielea kwenye mito  ya Pungue na Buzi iliyovunja kingo zake.

Picha: picture-alliance/dpa/D. Onyodi

Kimbunga cha idai kilichoandamana na upepo mkali uliopiga kwa kasi ya kilomita 160 kwa saa kilisababisha maporomoko ya ardhi nchini Msumbiji kabla ya kupungua kasi na kuelekea nchini Zimbabwe.

Kimbunga hicho kilianza kujikusanya mwanzoni mwa mwezi huu wa Machi  na kilikuwa tayari kimeshasababisha mafurukio nchini Malawi na msumbiji kwenyewe wiki kadhaa kabla ya kupiga kikamilifu. Wiki iliyopita maafisa kutoka nchi zote waliripoti kwamba watu 102 walijeruhiwa.

Kimbunga Idai kimeuharibu kabisa mji wa Beira ambako wafanyakazi wa mashirika ya msalaba mwekundu na hilali nyekundu wameripoti kwamba asilimia 90 ya majengo yameharibiwa kwa mujibu wa tathmini ya picha zilizopigwa kutokea angani.  Mji wa Beira wenye wakaazi kiasi laki tano hauna huduma za umeme tangu siku ya alhamisi wiki iliyopita wakati uwanja wa ndege ukifunguliwa tena siku ya jumapili.

Mamia kwa maelfu ya watu wanaishi bila umeme na huduma za simu au mawasiliano zote zimekatika katika maeneo mengi yaliyoathirika. Miji na vijiji chungunzima vimefunikwa na mafuriko nchini Msumbiji. Mkuu wa shirikisho la mashrika ya msaada ya kimataifa ya msalaba mwekundu na hilali nyekundu Jamie LeSueur amesema laini za mawasiliano zimekatika kabisa wakati  barabara nazo zikiharibika.Mkuu huyo wa IFRC amesema hali ni mbaya zaidi katika mji wa Beira ingawa pia wamepata taarifa kwamba huenda hali ikawa ni mbaya zaidi nje ya mji huo.

Picha: DW/M. Mueia

Inaarifiwa kwamba jumapili bwawa moja lilifurika na kuifunga kabisa barabara ya mwisho iliyokuwa imebakia ya kuingia mji huo. Mkoa wa Manicaland ni eneo ambalo pia lina hali ya kutisha kwa upande wa Zimbabawe huku mafuriko yakitishia kusababisha kutangazwa hali ya dharura ya kitaifa.Imeelezwa kwamba juhudi za kufikisha msaada katika maeneo yaliyoathirika zimeshindikana kufuatia barabara chungunzima kutopitika wakati madaraja nayo yamesombwa na mafuriko hayo.Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa mataifa WFP liliahidi kupeleka chakula kuwasaidia kiasi watu laki sita katika kanda hiyo.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW