Balaa la mashariki ya kati
18 Julai 2006
Tukianza na Mashariki ya kati, gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG likizungumzia azma ya Israel ya kuunda eneo la kujikinga na mashambulio kusini mwa Lebanon,laandika:
“Eneo la kinga –buffer zone- maana yake hasa ikiwa ndivyo inavyokusudiwa ni kulidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Lebanon,kuwapokonya silaha au kuwarudisha nyuma wafuasi wa Hozbollah,kuchukua dhamana kamili ya kusimamia usalama wa eneo hilo kubwa la mpakani.”
Kufanya hivyo,lasema gazeti, yamkini kukatuliza hali ya mambo kwa muda ,lakini kwa jicho la ghadhabu kubwa iliopo,hakutapunguza uwezekano wa kuzagaa kwa cheche za moto.
Ama gazeti la PFORZHEIMER ZEITUNG likigeukia juhudi za upatanishi linasema kuwa inaonesha kana kwamba pande zote mbili zimejiandaa kwa changamoto hii muda mrefu uliopita na sasa zinataka kuoneshana :
Israel,haioneshi iko tayari kuregeza kamba hadi kwanza imeteketeza sehemu kubwa ya makombora ya Hizbollah na Hizbollah nayo haiko tayari kurudi nyuma katika kuonesha jinsi gani tangu kupita siku kadhaa makombora yake yanavyopiga Israel.Kwa jicho la hali hii, yafaa kuuliza : juhudi zote za kupatanisha au za kupeleka vikosi vya UM zina maana gani ?
Kwa wakaazi wanaoteseka pande zote mbili za mpaka , kujiingiza kati kwa jamii ya kimataifa ni tumaini pekee-lasema FAZ.
Gazeti la GENERAL ANZEIGER linalochapishwa Bonn limegundua kuwa dharau ilioonesha Marekani kwa kuzitenga baadhi ya nchi za eneo hili:
Laandika:
“Wakati huu makosa mengi yaliofanywa na utawala wa Bush yamedhihirika.
Mojawapo ya makosa hayo kama inavyobainika wakati huu, ni kule kukataa kuzijumuisha Syria na Iran katika diplomasia ya Mashariki ya kati mnamo miaka michache iliopita.Kwani, nchi zote hizo mbili zikilaaniwa na rais Bush kuwa ni za kidikteta na sehemu ya mihimili ya uovu.Kumpumnga shetani wa Hizbollah na Hamas wakati huu wa jazba kali,kunawezekana tu kwa dawa mujarabu kutoka Teheran na Damascus.
Utawala wa Bush ukikataa katakata kuwa na mawasiliano na yeyote kati yao.
Likitubadilishia mada, gazeti la TAGESPOST linachambua mchango wa siku zijazo wa Urusi katika kundi la dola kuu 8-tajiri-G-8- baada ya kuwa mwenyeji wa mkutano huko st.Petersberg:
Laandika:
Kuuchagua pekee mji wa St.Petersberg kama kituo cha mkutano kumechangia kunyanyua zaidi heba ya Urusi.
Kambi ya magharibi haikuweza kumtilia dosari rais Putin katika mafanikio yake licha ya kukandamiza demokrasi nchini mwake.
Na hii ni busara kufanya ingawa Urusi tangu katika sera zake za ndani hata za nje inafaa kunyoshewa kidole.Dola za magharibi zitapaswa kujifunza jinsi ya kukabiliana na dola lenye kupata nguvu,lakini lisilo la kidemokrasi la Urusi-ni maoni ya TAGESPOST kutoka mjini Würzburg.