Balaa la njaa na jinsi ya kulipatia ufumbuzi magazetini
17 Machi 2017
Ufumbuzi wa kiufundi pekee hautoshi, wanakubaliana wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanaomnukuu katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiitaja kuwa "jinamizi" hali namna ilivyo katika pembe ya Afrika. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alizitembelea hivi karibuni nchi kadhaa za pembe ya Afrika. "Mabalaa yote yanakuja wakati mmoja: Mizozo, ukame, maradhi, amenukuliwa katibu mkuu Guterres akizungumzia hali namna ilivyo katika maeneo yanayokumbwa na mizozo ya Somalia, Nigeria na Sudan Kusini. Anasema hali hiyo inakumbusha balaa la njaa la miaka ya nyuma ambalo wengi waliamini lisingeweza tena kutokea. Kutokana na hali namna ilivyo jumuia ya kimataifa inabidi iwajibike haraka bila ya kujali sababu za hali hiyo.
Ili kuepukana na balaa jengine kama hilo suala la kutaka kujua chanzo ni muhimu anaandika mhariri wa gazeti la Die Zeit anaehisi serikali za Afrika zinabeba jukumu kwa njia moja au nyengine kwa yanayotokea .
Umuhimu wa kuundwa fuko maalum kugharimia majanga kabla hayajatokea
Gazeti la die tageszeitung linazungumzia kuhusu mpango wa misaada ambao hauungwi mkono. Linasema waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller anapendekeza pawepo kituo maalum cha kusimamia misaada. Suala kama serikali kuu itauunga mkono mpango huo, bado halijapatiwa jibu linaandika gazeti la die tageszeitung. "Nani anaweza kumbisha waziri wa misaada ya maendeleo Gerd Müller? Mara nyingi misaada inapofika, maji yanakuwa yameshazidi unga. Umoja wa mataifa unabidi uwe na uwezo wa kusimamia majanga kabla hayajatokea" analalamika waziri huyo wa kutoka chama cha Christian Social Union-CSU, kutokana na balaa la ukame na njaa Afrika Mashariki. Anashauri liundwe fuko la dala bilioni 10 linaloweza kuingilia kati haraka ikihitajika. Die Tageszeitung linamaliza kwa kusema hata kama fikra ya waziri Gerd Müller ni nzuri, lakini hadi wakati huu bado serikali kuu haijaamua kuiunga mkono.
Nishati ya juwa ni muhimu zaidi kwa Afrika
Nishati ya juwa kwa Afrika ndio kichwa cha maneno cha gazeti la Der Tagesspiegel linalilozungumzia kuhusu tume ya ushauri inayoongozwa na katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan.Tume hiyo inajaribu kuzishauri serikali za Afrika zitangulize mbele nishati ya juwa na kuusimamia wenyewe mradi huo.Waafrika milioni 620 hawawezi kusubiri hadi mitambo ya nishati ya juwa itakapoundwa, amenukuliwa Kofi akisema mjini Abidjan, nchini Côte d'Ivoire alipokuwa akiwasilisha ripoti ya jopo la maendeleo barani Afrika-ambalo yeye ndie mwenyekiti wake. Kauli mbiu ya ripoti hiyo "Anaetaka kuleta umeme Afrika, anabidi ashughulikie nishati ya juwa".Tena bila ya kusubiri mitambo mikubwa ya kusambaza nishati hiyo. Badala yake ripoti ya katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa inahimiza mitambo midogo midogo itakayotumika kwa daraja ya mikoa-inayojulikana kwa lugha ya kitaalamu kama "Mini-Grads". Waasisi wa ripoti hiyo kuhusu nishati ya juwa kwa bara la Afrika wanazungumzia hatua tatu muhimu: Ya mwanzo inahusu bei hafifu ya nishati ya juwa. Wanahisi ni rahisi zaidi kwa watu walio maskini wanaoishi vijijini na mijini kununua taa inayotumia nishati ya juwa, badala ya dala 180 wanazotoa kwa mwaka kununua mishumaa, kujaza taa za kibatari mafuta au kununua betri za taa za mikononi. Taa ya nishati ya juwa inagharimu siku hizi chini ya dala tano.
Mtindo wa kutumia fedha taslimu unaanza kutoweka Afrika
Ripoti yetu ya mwisho inazungumzia jinsi simu za kimambo leo Smartphone zinavyobadilisha desturi za maisha. Berliner Zeitung linasema mazoweya ya watu kutumia fedha taslim yanaanza kutoweka na badala yake watu wanavutiwa zaidi na kulipa kupitia Apps.Gazeti linazungumzia utaratibu ulioanzishwa na raia wawili wa Kenya mnamo mwaka 2007, M-Pesa unaorahisisha watu kulipa na kulipia bila ya fedha taslim. Hata hivyo Berliner Zeitung linasema utaratibu huo una ila zake, nazo ni kwamba data za watu hazibakii mahala pa moja.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/ BASIS/PRESSER/ALL/PRESSE
Mhariri: Iddi Ssessanga