1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Balozi wa Marekani, asusia kumbukumbu ya bomu Japan

9 Agosti 2024

Balozi wa Marekani nchini Japan Rahm Emanuel amesusia hafla iliyoandaliwa leo ya kumbukumbu ya miaka 79 ya shambulio la bomu la Atomiki mjini Nagasaki.

Rahm Emanuel
Picha: Hidetaka Ando/Jiji Press/dpa/picture alliance

Uamuzi wa balozi huyo kususia hafla hiyo umetokana na kutoalikwa kwa balozi wa Israel kwenye hafla hiyo.

Badala yake, Rahm Emanuel amehudhuria mkutano wa maombi katika Sinagogi la Tokyo akiwa pamoja na balozi wa Israel nchini humo Gilad Cohen na mwenzake wa Uingereza Julia Longbottom, ambaye pia amesusia hafla hiyo.

Meya wa Nagasaki Shiro Suzuki hata hivyo amesisitiza kuwa, kutohudhuria kwa Cohen katika hafla hiyo ya kila mwaka sio kwa sababu za kisiasa bali ni kuepusha maandamano yanayoweza kutokea juu ya vita vinavyoendelea katika ukanda wa Gaza.

Mnamo Agosti 9 mwaka 1945, Marekani ilirusha bomu la Atomiki mjini Nagasaki na kusababisha vifo vya watu 74,000 wakiwemo manusura wengi waliokufa baadaye kutokana na athari ya mionzi ya bomu hilo.