Balozi wa Ujerumani Chad atakiwa kuondoka
10 Aprili 2023Balozi wa Ujerumani nchini Chad, Jan-Christian Gordon Kricke, amewasili mjini Berlin baada ya kufukuzwa kutoka taifa hilo la Afrika ya Kati. Taarifa hii ni kwa mujibu wa vyanzo vya Shirika la Habari la Ujerumani-DPA.
Awali Jumamosi Kricke alionekana akiwa na mabalozi kadhaa wa mataifa rafiki kwenye uwanja wa ndege wa N'Djamena, baada ya serikali kumtangaza kuwa mtu asiyehitajika na kumtaka kuondoka nchini humo ndani ya masaa 48.
Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Chad, uamuzi wa kumtimua balozi huyo unatokana na kile ilichosema tabia ya utovu wa nidhamu ya kushindwa kuheshimu taratibu za kidiplomasia kwa zingatio la Mkataba wa Vienna. Hakukuwa na ufafanuzi zaidi.
Dawati la mambo ya nje la Ujerumani limesema sababu ya balozi huyo kufukuzwa haikuwa wazi, na kuongeza kuwa inawasiliana na serikali nchini Chad ili kupata maelezo ya kina.