1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban asikitika baada ya CPJ kunyimwa hadhi UN

28 Mei 2016

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesikitishwa kwa kiasi kikubwa na hatua ya Umoja wa Mataifa kuinyima hadhi maalum Kamati ya Kuwalinda Wanahabari – CPJ katika shirika hilo la kimataifa

CPJ Commitee to protect Journalists
Picha: picture alliance/AP Photo

Kamati moja ya Umoja wa Mataifa ilipiga kura Alhamisi kupinga ombi la kamati hiyo ya kutetea uhuru wa wanahabari la kupewa kibali cha kuwa shirika lisilo la kiserikali. Wanakamati 10 walipiga kura ya kupinga wakati sita wakikubali ombi hilo na watatu hawakupiga kura.

Ban “anaamini kuwa wanahabari wanafanya kazi bora” na “amesikitika kabisa” kutokana na uamuzi huo, ambao utaizuia kamati ya kuwalinda wanahabari – CPJ kuzifikia taasisi za Umoja wa Mataifa, likiwemo Baraza la Haki za Binaadamu lenye makao yake mjini Geneva, alisema msemaji wake Farhan Haq. “wanahabari tayari wanakabiliwa na vikwazo visivyofaa katika kazi yao katika maeneo mengi ulimwenguni na mashirika ambayo yamejitolea kuwalinda wanahabari hayapaswi kukabiliwa na vizuizi katika Umoja wa Mataifa” aliongeza.

Urusi, China, Sudan na Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi 10 ambazo zilipiga kura kupinga ombi la CPJ kupewa hadhi maalum ya ushauriano katika shirika hilo la kimataifa. Marekani, ambayo ilipiga kura ya kuunga mkono, ilisema italeta ombi hilo la CPJ mwezi Julai katika kikao kizima cha Baraza la Kiuchumi na Kijamii – ECOSOC lenye nchi wanachama 54 kujaribu kuubatilisha uamuzi huo.

Picha: APTN

Katika hatua ya kurudi nyuma, Afrika Kusini imesema inaunga mkono ombi la CPJ na itapiga kura ya kuliunga mkono wakati litakapowasilishwa katika kikao cha ECOSOC.

“Tunasikitika kuhusu kuchukuliwa vibaya na ujumbe mbaya ambao ukosefu wa ufafanuzi wa kura yetu katika kamati la mashirika yasiyo ya kiserikali – NGO huenda umeonyesha” imesema taarifa kutoka kwa idara ya mahusiano ya kimataifa ya Afrika Kusini. Afrika Kusini imeisifu CPJ kwa “kazi yake ya kipekee na bora zaidi” na ikasema inaunga mkono “jukumu ambalo wanahabari wanatekeleza katika jamii zenye demokrasia na zilizo huru”.

Azerbaijan, Burundi, Cuba, Nicaragua, Pakistan na Venezuela pia zilipinga ombi la CPJ, ambalo limeangazia kadhia ya wanahabari waliokamatwa na kufungwa jela kote duniani wakati wakiripoti matukio mbalimbali.

Wanadiplomasia wanasema kura hiyo ilionyesha pingamizi linaloongezeka dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali katika Umoja wa Mataifa, hasa yale yanayotetea haki za uzazi na yanayopaza sauti kuhusu masuala ya mashoga na uhuru wa kujieleza.

Mapema mwezi huu, karibu mashirika 20 yasiyo ya kiserikali, mengi ambayo huzungumzia haki za mashoga, yalizuiwa kushiriki katika mkutano muhimu wa Ukimwi mwezi Juni baada ya nchi 51 za Kiislamu, Urusi na mataifa ya Afrika kulalamika.

Mwandishi wa ripoti maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za uhuru wa kukusanyika kwa amani na kushirikiana, Maina Kiai wa Kenya, alisema ni serikali hizo hizo zinazoyazuia makundi ya kiraia katika nchi zao na sasa zinaulenga Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo