Ban Ki-Moon ahofia Al-qaeda kuingia Syria
18 Mei 2012Ban Ki-Moon amesema pia kuwa rais Bashar Assad bado hajatekeleza mpango wa amani wa Koffi Annan uliokubaliwa na Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za Kiarabu.
Katibu Mkuu Ban Ki-Moon aliuambia Mkutano wa vijana uliofanyika katika Makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuwa ushiriki wa Al-qaeda katika mgogoro wa Syria unasababisha matatizo makubwa zaidi na kwamba hali ilivyo sasa hivi haivumiliki hata kidogo.
"Siku chache zilizopita kulitokea shambulio kubwa. Naamini lazima Al-qaeda walihusika na shambulio hili na pia kulikuwa na mashambulizi mara mbili dhidi ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa na kwa hivyo tunajitahidi kadiri ya uwezo wetu kulinda usalama wa raia," alisema Ban.
Syria nayo yaitupia lawama Al-qaeda
Syria imekuwa ikilishtumu kundi la Al-qaeda kwa kuhusika na mashambulizi makubwa katika wiki za hivi karibuni kama lile la Mei 10 lililosababisha vifo vya takribani watu 55 na kujeruhi wengine wapatao 400. Maafisa nchini Marekani na Urusi nao wanaamini Al-qaeda na makundi mengine ya wanamgambo wamejipenyeza ndani ya Syria.
Mwezi huu, Syria ilituma barua kwenda Umoja wa Mataifa ikiwa na majina ya watu 26 iliyowateka, wengi wao wakiwa raia wa Tunisia na Libya na kwa mujibu wa barua hiyo, 20 kati ya watu hao walikiri kuwa wanachama wa kundi la Al-qaeda.
Katibu Mkuu huyo pia alizungumzia mchango wa timu ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa nchini humo ambayo ndiyo hatua ya kwanza kutekelezwa kati ya sita za Mpamgo wa amani wa Kofi Annan.
Kiongozi wa waangalizi ataka majadiliano
Wakati huo huo, kiongozi wa timu ya waagalizi, Meja Jenerali Robert Mood amesema hakuna idadi ya waangalizi itakayofanikisha amani ya kudumu nchini Syria bila ya kuwepo majadiliano. Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari mjini Damascus, Mood ameziomba pande zote katika mgogoro huu kuacha kushambuliana na kutoa nafasi kwa timu yake kujenga mazingira ya majadiliano.
Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinasema bomu lililopuka Ijumaa asubuhi katika mkoa wa Aleppo lilimuua mwanajeshi mmoja na kuwajeruhi wengine watano, kwa mujibu wa shirika la uangalizi wa haki za binadamu nchini Syria.
Siku ya Ijumaa wanaharakati waliitisha mandamano kuunga mkono wanafunzi wa chuo Kikuu cha Aleppo waliofyatuliwa risasi usiku wa Alhamis wakati walipokuwa wakishiriki maandamano ya kuupinga utawala wa rais Assad.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\DPAE\APE\AFPE
Mhariri: Josephat Charo Nyiro