1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BANGKOK : Uchaguzi mwaka 2007

20 Septemba 2006

Mkuu wa majeshi nchini Thailand aliyeipinduwa nchi hiyo hapo jana bila ya kumwaga damu ameahidi kuitisha uchaguzi kufikia mwezi wa Oktoba mwaka 2007 na kudokeza kwamba Waziri Mkuu aliepinduliwa madarakani Thaksin Shinawatra yumkini akafunguliwa mashtaka.

Generali Sondhi Boonyaratkalin ameongoza mapinduzi hayo wakati wa usiku bila ya kufyetuwa risasi hewani na kuwapeleka wanajeshi na vifaru kulinda maeneo muhimu na kuzingira majengo ya serikali wakati Waziri Mkuu huyo mashuhuri Thaksin anayetuhumiwa kwa rushwa na kudhoofisha asasi za demokrasia akiwa mjini New York kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Wakati alipoulizwa iwapo hatua zitachukuliwa kutaifisha mali za Thaksin mkuu huyo wa majeshi ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba wale waliofanya makosa watashtakiwa kwa mujibu wa sheria lakini hakufafanuwa zaidi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Thailand TNA Waziri Mkuu aliepinduliwa amesema katu hakutegemea kwamba jeshi litafanya mapinduzi na amedokeza kwamba hangelijaribu kun’gan’gania madaraka.

Thaksin tayari ameondoka New York kuelekea London kwa ziara binafsi akiandamana na Naibu Waziri Mkuu Surakiart Sathiratai ambaye alitowa wito wa kuchukuliwa hatua ya kulinda demokrasia.

Mkuu wa Majeshi wa Thailand amesema atakaimu Uwaziri Mkuu kwa wiki mbili hadi hapo kiongozi mpya atakapopatikana.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW