1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Janga

Bangladesh yatangaza kifo cha kwanza cha COVID 19

2 Juni 2020

Bangladesh imetangaza kifo cha kwanza kilichosababishwa na virusi vya corona katika makambi ya wakimbizi yaliyoko kusini mwa Bangladesh, maafisa wamesema Jumanne. (02.05.2020)

Bangladesch Symbolbild Rohingya-Flüchtlingslager in Cox's Bazar
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Swarup

Mtu huyo aliyefariki ni mzee wa jamii ya Rohingya mwenye umri wa miaka 71. Alifariki Mei 31 wakati akiwa anapatiwa matibabu kwenye kituo cha kujitenga, amesema Bimal Chakma, afisa mwandamizi wa tume za kuwasaidia na kuwawezesha wakimbizi.

Takriban warohingya 29 wamepatikana na maambukizi ya virusi vya corona tangu kisa cha kwanza kilipogundulika Mei 14. Maafisa wamesema watu 339 wamepimwa hadi sasa miongoni mwa wakimbizi wanaoishi kwenye makambi hayo. Bangladesh imeripoti visa 52,445 vya virusi vya corona na vifo 709.

Watoa huduma za afya wameonya kuhusu janga kubwa la kibinaadamu iwapo kutatokea mripuko mkubwa kwenye kambi hizo za wakimbizi, zilizoko nje ya mji wa Cox Bazar ambako wanaishi mamilioni ya wakimbizi wa Rohingya, wengi miongoni mwao wakiwa ni waislamu wa jamii ya wachache waliokimbia hatua za kikatili za jeshi la Myanmar.

Mwanajeshi akiendesha kampeni ya kujenga ufahamu kuhusu covid-19 miongoni mwa wakimbizi wa jamii ya Rohingya nchini Bangladesh.Picha: DW/Abdur Rahman

Ripoti mpya ya WHO yaonyesha wagonjwa wengine kusahaulika

Katika hatua nyingine, shirika la afya ulimwenguni, WHO limetoa ripoti siku ya Jumanne ikionyesha namna janga la corona lilivyoathiri pakubwa matibabu ya maradhi mengine kote ulimwenguni.

Kulingana na utafiti wake kwenye mataifa 155 mwezi uliopita, shirika hilo la afya liligundua kwamba watu wanaougua magonjwa yasiyo ya kuambukiza, wengi miongoni mwao wako katika hatari kubwa ya matatizo ya kiafya yanayosababishwa na COVID-19, hawapati huduma bora pamoja na dawa wakati wa janga hilo.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema "uchunguzi unaonyesha kwamba wengi wa watu hao wanahitaji matibabu ya magonjwa kama saratani, maradhi ya moyo na kisukari wamekuwa hawapati matibabu na dawa wanazozihitaji tangu janga hilo lilipoanza.”

Utafiti huo wa WHO unaonyesha kwamba 31% ya mataifa yalilazimika kuzuia ama kusimamisha kabisa huduma za magonjwa ya moyo, 42% waliondosha huduma kwa wagonjwa wa saratani, 49% kwa wagonjwa wa kisukari na zaidi ya nusu walishindwa kuendeleza huduma kwa wagonjwa waliokuwa na shinikizo la damu.

Ripoti hiyo imesema zaidi ya asilimia 90, watumishi wa afya walipewa jukumu la kushughulikiwa wagonjwa wa corona. Vizuizi vinavyohusiana na mzozo huu pia vilichangia kufutwa kwa ahadi za kukutana na madaktari ama watoa huduma za afya.

Mfanyakazi wa afya akiwa amevaa vyazi ka kujikinga katika kambi ya wakimbi wa Rohingya ya Kutupalong, katika wilaya ya Cox's Bazar, Aprili 15,2020.Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Rahman

Hali yazidi kuwa tete Amerika ya Kusini

Kwingineko duniani, Uhispania imetangaza kutokuwa na kifo chochote cha virusi vya corona ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwezi Machi. Huku Italia ikitangaza kiwango cha chini kabisa cha ongezeko la kila siku la wagonjwa wa COVID-19 tangu mapema mwezi Machi, kabla ya kuchukuliwa hatua ya kusimamisha kabisa shughuli nchini humo.

Kulingana na WHO, Amerika ya Kusini kwa sasa ndio inashuhudia mtikisiko mkubwa zaidi wa virusi vya corona ulimwenguni, ingawa amesema bado hawawezi kukadiria ni wakati gani watafikia kiwango cha juu kabisa cha maambukizi.

WHO kupitia mkuu wa kitengo cha dharura Dr. Michael Ryan imesema katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, mataifa matano kati ya 10 yaliyoripoti idadi ya juu kabisa ya maambukizi ni Marekani, Brazil, Peru, Chile na Mexico.

Vyanzo: DW,RTR,AP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW