1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taifa Stars yalazimishwa sare ya 1-1 na Zambia

22 Januari 2024

Mshambuliaji wa Zambia Patson Daka alifunga bao la dakika za mwisho na kuisadia timu hiyo iliyokuwa na wachezaji kumi kutoka sare ya 1-1 na Tanzania, na kuwanyima wapinzani wao ushindi wa kwanza kwenye mechi ya kundi F.

Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON | Uwanja wa Alassane Ouattara
Uwanja wa Alassane Ouattara mjini AbidjanPicha: Braima Darame/DW

Simon Msuva aliiweka kifua mbele Tanzania kunako dakika ya 11 ya mchezo katika uwanja wa Laurent Pokou japo bao la kichwa la Daka katika dakika 88 kulifanya timu hizo kugawanya alama.

Tanzania, Taifa Stars ilianza kampeni ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON kwa kufungwa mabao 3-0 na Morocco.

Katika mechi nyingine, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilitoka sare ya 1-1 na Morocco.

Matokeo hayo yanaiacha Morocco kuwa kileleni mwa kundi F ikiwa na alama nne, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia zina alama mbili wakati Tanzania inaburuta mkia ikiwa na alama moja tu, baada ya michezo miwili.

Soma pia: Nyota wa Misri Mohamed Salah kuzikosa mechi mbili za AFCON kutokana na jeraha

Tanzania ilikuwa imeshindwa kupata ushindi katika mechi zao za awali katika michuano ya mwaka 1980 na 2019, na hawakupewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano ya AFCON mwaka huu hasa baada ya kocha wao Adel Amrouche kufungiwa mechi nane siku ya Ijumaa.

Shamrashamra za Kongo kuelekea mechi ya AFCON

02:47

This browser does not support the video element.

Adhabu hiyo ilitolewa na kamati ya nidhamu ya CAF, malalamiko yaliyowasilishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (RMFF) dhidi ya kocha Amrouche.

RMFF ilimlalamikia Kocha huyo kwa kauli zake kuwa Morocco ina ushawishi ndani ya CAF katika kupanga mechi pamoja na waamuzi.

Tanzania imemteua Hemed Morocco kuwa kaimu kocha akisaidiwa na Juma Mgunda.