1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bara la Afrika laazimia kuagiza dawa ya kutibu COVID-19

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
13 Januari 2022

Shirika linalosimamia afya ya umma barani Afrika linafanya mazungumzo na kampuni ya Pfizer kuhusu bara hilo kuagiza dawa ya kumeza inayoitwa Paxlovid ya kutibu COVID-19.Dawa hiyo ina ufanisi wa karibu asilimia 90.

John Nkengasong | Director of the Africa Centers for Disease Control and Prevention
Picha: Mulugeta Ayene/AP/picture alliance

Kwa mujibu wa data kuhusianna na dawa hiyo inayoitwa Paxlovid imebainika kwamba inaweza kuepusha vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa COVID-19. Mkurugenzi wa vitengo vya kudhibiti magonjwa barani Afrika CDC, John Nkengasong, amesema kwa sasa wanafanya majadiliano ya karibu na kampuni ya Pfizer ili kuwezesha upatikinaji wa dawa hizo.

John Nkengasong: Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani AfrikaPicha: Mulugeta Ayene/AP/picture alliance

Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza ulazima kwa watu wazima wote kupata chanjo za COVID-19. Wabunge wa vyama mbalimbali walipiga kura kuunga mkono hatua hiyo kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya corona isipokuwa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha (AfD) ambacho takriban nusu ya wabunge wake hawakuhudhuria kikao cha bunge kilichofanyiak siku ya Jumatano ambapo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kujibu maswali ya wabunge.

Nchini Ufaransa baraza la Seneti limeidhinisha hatua mpya za kukabiliana na virusi vya corona pamoja na matumizi ya pasi ya kidijitali inayoonyehsa kuwa mtu amepata chanjo. Wakati huo huo walimu wameandamana kwenye miji mbalimbali kote nchini Ufaransa kupinga sera ya serikali kuhusiana na maambukizi ya virusi vya corona na taarifa zaidi zinafahamisha kuwa waziri wa Afya wa Ufaransa Olivier Veran amethibitishwa kuwa na COVID-19.

Kansela wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: Hannibal Hanschke/REUTERS

Kwingineko masoko ya hisa barani Ulaya yaliporomoka leo hii huku sekta ya ujenzi ikiwa miongoni mwa sekta zilizoathirika kwa hisa zake kushuka kutokana na wasiwasi unaosababishwa na kuendelea kuongezeka kwa idadi ya watu wanaougua COVID-19, dalili inayoashiria tunaelekea kwenye mazingira ya kubana mkanda katika sera ya fedha.

Huko nchini Uingereza Naibu mkuu wa matibabu Jonathan Van-Tam, ametangaza leo kuwa anajiuzulu jukumu hilo na kurejea kwenye Maisha ya kitaaluma. Anatarajiwa kurejea katika Chuo Kikuu cha Nottingham, ambapo amekuwa anahudumu tangu mwaka 2017. Van-Tam, alitunukiwa heshima ya ushujaa na Malkia Elizabeth mnamo mwaka mpya kwa kutambua huduma na mchango wake mkubwa katika mapambano dhidi ya janga la corona amesema "Sote tunatamani COVID-19” na ameshukuru kwa kupewa nafasi hiyo ambapo aliwatumikia watu wa Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: House of Commons/PA via AP/picture alliance

Tangazo la kujiuzulu kwake amelitoa siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson kuomba msamaha kutokana na kukiuka sheria kwa kuruhusu hafla iliyofanyika kwenye makazi yake rasmi ya Downing Street nambari 10 wakati wa karantini ya kwanza nchini humo wakati ambapo watu walikuwa hawaruhusiwi kukusanyika kwenye makundi.

Chanzo:RTRE/ https://p.dw.com/p/45Ree

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW